35. Kuwa na subira kwa makadirio ya Allaah ni katika kumuamini Allaah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ يَهْدِ قَلْبَهُ ۚ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Hausibu msiba wowote [kukupateni] isipokuwa kwa idhini ya Allaah. Yeyote   anayemuamini Allaah, basi huuongoza moyo wake. – Allaah kwa kila kitu ni mjuzi.” (at-Taghaabuun 64:11)

´Alqamah amesema:

“Huyo ni yule mtu ambaye anapofikwa na msiba anajua kuwa umetoka kwa Allaah, basi akaridhika na akajisalimisha.”

2- Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mambo mawili kwa watu ni kufuru; kutukaniana nasabu na kuomboleza juu ya maiti.”[1]

3- al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Si katika sisi yule mwenye kujipiga kwenye mashavu, akachana nguo na akaita kwa mayowe ya kipindi cha kikafiri.”[2]

4- Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah anapomtakia mja Wake kheri, basi humharakishia adhabu duniani, na anapomtakia mja Wake shari, humcheleweshea adhabu ya dhambi yake mpaka siku ya Qiyaamah.”[3]

5- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ukubwa wa malipo ni pamoja na ukubwa wa mitihani. Hakika Allaah (Ta´ala) anapowapenda watu basi huwapa huwajaribu. Yule mwenye kuridhia basi hupara radhi Zake na yule mwenye kuchukia basi hupata hasira Zake.”[4]

Ni nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy.

MAELEZO

Mwandishi alichotaka ni kubainisha kwamba kuwa na subira juu ya makadirio ya Allaah ni katika imani na kwamba ni wajibu kwa muumini kutokata tamaa wakati anapofikwa na msiba kwake mwenyewe, mwana wake, mali yake au familia yake. Anachotakiwa ni yeye kuvuta subira. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ

”Bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu kidogo katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao [ya kazi zenu]. Wabashirie wenye kusubiri ambao unapowafika msiba basi husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” (al-Baqarah 02:155-156)

وَاصْبِرُوا ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ

“Subirini! Hakika Allaah yupamoja na wenye kusubiri.”  (al-Anfaal 08:46)

إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ

“Hakika wale wenye kusubiri watalipwa kikamilifu ujira wao pasi na hesabu.” (az-Zumar 39:10)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule ambaye atafanya subira basi Allaah atamsubirisha. Hakuna yeyote aliyepewa zawadi bora na pana kama subira.”[5]

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ يَهْدِ قَلْبَهُ ۚ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Hausibu msiba wowote [kukupateni] isipokuwa kwa idhini ya Allaah. Yeyote   anayemuamini Allaah, basi huuongoza moyo wake. – Allaah kwa kila kitu ni mjuzi.”

´Alqamah amesema:

“Huyo ni yule mtu ambaye anapofikwa na msiba anajua kuwa umetoka kwa Allaah, basi akaridhika na akajisalimisha.”

Bi maana anaamini kwamba Allaah ndiye kapanga na ndiye kakadiria msiba huu ambapo akavuta subira pasi na kukata tamaa. Kwa sababu ya kitendo chake kizuri Allaah anauongoza moyo wake katika kheri, anamtuliza na kumfanya imara. ´Alqamah amesema:

“Huyo ni yule mtu ambaye anapofikwa na msiba anajua kuwa umetoka kwa Allaah, basi akaridhika na akajisalimisha.”

2- Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mambo mawili kwa watu ni kufuru; kutukaniana nasabu na kuomboleza juu ya maiti.”

Bi maana kuzitweza koo [za watu] kwa sababu ya kiburi, jeuri kwa watu na kuwadharau. Ni aina fulani ya kufuru, lakini ni aina ya kufuru ndogo na sio kubwa. Kitendo hichi ni miongoni mwa mambo ya kipindi cha kikafiri. Katika ile Hadiyth iliotangulia imekuja:

“Mambo mane katika Ummah wangu ni miongoni mwa mambo ya kipindi cha kikafiri na hawatoyaacha; kujifakhari kwa unasabu, kutukaniana nasabu, kuinasibisha mvua kwa nyota na kuomboleza.”

Ama ikiwa makusudio ni kuwatambulisha watu fulani, hakuna neno na hakuingii katika Hadiyth.

Kuomboleza juu ya maiti kunafahamisha kukata tamaa na ndani yake kuna kunyanyua sauti juu. Haijuzu. Ama kutiririkwa na machozi, kwa msemo mwingine kulia, hakuna neno. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Macho yanatokwa na machozi na moyo unahuzunika na hatusemi isipokuwa yale yenye kumridhisha Mola wetu. Hakika ni wenye kuhuzunika kwa kutengana na wewe Ibraahiym.”[6]

 3- al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Si katika sisi yule mwenye kujipiga kwenye mashavu, akachana nguo na akaita kwa mayowe ya kipindi cha kikafiri.”[7]

Haya yanafahamisha kukata tamaa na ni katika matendo ya kipindi cha kikafiri. Ni wajibu kuwa na subira na kutambua kuwa Allaah ndiye kayakadiria makadirio haya. Pamoja na kuwa kifo hakiepukiki mtu anatakiwa kufanya zile sababu zinazokubaliana na Shari´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi niko mbali kabisa na mwanamke anayenyanyua sauti yake, mwenye kuzinyoa nywele zake na  mwenye kuzipasua nguo zake wakati wa msiba.”[8]

4- Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah anapomtakia mja Wake kheri, basi humharakishia adhabu duniani, na anapomtakia mja Wake shari, humcheleweshea adhabu ya dhambi yake mpaka siku ya Qiyaamah.”

Akitaka kumfutia mja madhambi yake basi humharakishia adhabu hapa duniani ima kwa kumpa ufakiri, kumpa magonjwa, kuharibika kw mali yake na mfano wake. Kwa njia hiyo Allaah anamfutia madhambi yake na mambo yake mabaya. Anapomtakia shari basi humwacha akatenda madhambi na akamcheleweshea adhabu ya madhambi yake mpaka siku ya Qiyaamah. Adhabu ya Aakhirah ni mbaya zaidi kuliko ya duniani. Mitihani mingi ya duniani kuna uwezekano ikawa ni sababu ya kusamehewa na kufutiwa madhambi. Kwa ajili hiyo ndio maana mtu anatakiwa kuwa na subira.

5- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ukubwa wa malipo ni pamoja na ukubwa wa mitihani. Hakika Allaah (Ta´ala) anapowapenda watu basi huwapa huwajaribu. Yule mwenye kuridhia basi hupara radhi Zake na yule mwenye kuchukia basi hupata hasira Zake.”

Ni nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy.

Jinsi mtihani utakuwa mkubwa ndivo malipo yanavyokuwa makubwa zaidi. Jinsi maradhi yanavyokuwa makali ndivo mtu anavyosamehewa zaidi. Jinsi msiba katika mali ya mtu ni mkubwa au vyenginevyo ndivo malipo na thawabu zinavyokuwa nyingi zaidi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah (Ta´ala) anapowapenda watu basi huwapa huwajaribu.”

Anawajaribu watu ili awafuatie madhambi yao na kuwaondoshea mambo yao maovu hadi pale wanapokutana Naye wanakuwa safi na matokeo yake wanaingia Peponi pale mwanzoni mwanzoni. Mfano wa Hadiyth kama hiyo ni maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Watu wenye mitihani mizito kabisa ni Mitume, kisha wenye kufanana nao, kisha wenye kufanana nao. Mtu anapewa majaribio kwa kiasi cha dini yake.”[9]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Watu wenye mitihani mizito kabisa ni Mitume, kisha watu wema, kisha wenye kufanana nao, kisha wenye kufanana nao. Mtu anapewa majaribio kwa kiasi cha dini yake.”[10]

Dini ya mtu ikiwa na nguvu ndivo anavyopewa majaribio zaidi.

[1] Muslim (67).

[2] al-Bukhaariy (1294) na Muslim (103).

[3] at-Tirmidhiy (2396), al-Haakim (8799) na Abû Ya´laa (4254). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (308).

[4] at-Tirmidhiy (2396) na Ibn Maajah (4031). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (2110).

[5] al-Bukhaariy (1469) na Muslim (1053).

[6] al-Bukhaariy (1303) na Muslim (2315).

[7] al-Bukhaariy (1294) na Muslim (103).

[8] al-Bukhaariy kwa cheni ya wapokezi iliopungua na Muslim (104).

[9] at-Tirmidhiy (2398), Ibn Hibbaan (2900), al-Haakim (121) na al-Bayhaqiy (6326). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahyh-ul-Jaami´” (994).

[10] Ahmad (1481). Nzuri kwa mujibu wa Shu´ayb al-Arnaa’uut.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 115-117
  • Imechapishwa: 24/10/2018