35. Je, inajuzu kupangusa juu ya soksi mtu akizivua ilihali yuko na wudhuu´ kisha akazivaa tena kabla ya kuchenguka wudhuu´ wake?

Swali 35: Je, inajuzu kupangusa juu ya soksi mtu akizivua ilihali yuko na wudhuu´ kisha akazivaa tena kabla ya kuchenguka wudhuu´ wake?

Jibu: Akivua soksi kisha akazivaa tena ilihali bado yuko na wudhuu´ basi hatoki nje ya hali zifuatazo:

1 – Ikiwa huu ni ule wudhuu´ wa kwanza au kwa msemo mwingine ikiwa wudhuu´ wake haujachenguka baada ya kuzivaa, ni sawa akazivaa tena  na akapangusa juu yake pale atapotawadha.

2 – Ikiwa wudhuu´ huu ni ule ambao alipangusa juu ya soksi, haijuzu kwake atapozivua akazivaa tena na kupangusa juu yake. Kwa sababu ni lazima azivae baada ya kujitwahirisha kwa maji. Twahara aliyofanya yeye ni kwa njia ya kupangusa. Haya ndio yanayotambulika kutoka katika maneno ya wanazuoni. Lakini hata hivyo ikiwa kuna aliyesema kuwa akirudi kuzivaa tena katika hali ya twahara – hata kama itakuwa ni twahara kwa njia ya kupangusa – ana ruhusa ya kupangusa midhali bado kumebaki muda wa kupangusa. Maoni haya ndio yenye nguvu hata kama sijui kuna yeyote aliyesema hivi. Kinachonizuia kusema maoni haya ni kwa sababu sijaona yeyote aliyesema hivi. Ikiwa kuna mwanachuoni yeyote aliyesema hivi, basi hii ndio maoni ninayoonelea kuwa ni ya sawa. Kwa sababu twahara ya kupangusa ni twahara kamilifu. Hivyo inatakikana kusema, akipangusa juu ya kile alichokivaa katika hali ya twahara ya kuosha basi ni sawa vilevile kupangusa juu ya kile alichokivaa katika twahara ya kupangusa. Lakini hata hivyo sijaona yeyote aliyesema hivi na Allaah ndiye mjuzi zaidi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Buhuuth wa Fataawaa fiyl-Mas´h ´alaal-Khuffayn, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (11/178-179)
  • Imechapishwa: 06/05/2021