34. Ni ipi hukumu ya kupeana mikono baada ya kumaliza kuswali?

Swali 34: Ni ipi hukumu ya kupeana mikono baada ya kumaliza kuswali? Je, kuna tofauti kati ya swalah ya faradhi na swalah iliyopendekezwa?

Jibu: Kimsingi na kusuniwa ni kupeana mikono wakati wanapokutana waislamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akipeana mikono na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum) anapokutana nao. Walikuwa wakipeana mikono wakati wanapokutana. Anas (Radhiya Allaahu ´anh) na Sha´biy (Rahimahu Allaah) wamesema:

“Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakipeana mikono pindi wanapokutana na wakikumbatiana pindi wanapofika kutoka safarini.”

Vilevile imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kwamba Twalhah bin ´Ubaydillaah (Radhiya Allaahu ´anh), mmoja katika wale kumi waliobashiriwa Pepo, alisimama kutoka katika mzunguko wa kielimu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwelekea Ka´b bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) – wakati Allaah alipomkubalia tawbah yake – ambapo akampa mkono na akampongeza kwa tawbah. Hili ni jambo linalotambulika kati ya waislamu katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na baada yake. Vilevile imethibiti kuwa amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna waislamu wawili wanaokutana ambapo wakapeana mikono isipokuwa yanapukuchika madhambi yao kama ambavo mti unapukuchisha majani yake.”

 Inapendekezwa kupeana mikono wakati wa kukutana msikitini au katika safu. Wasipowahi kupeana mikono kabla ya swalah basi watapeana mikono baada yake kwa ajili ya kuhakiki Sunnah hii tukufu. Isitoshe jambo hilo linathibitisha mapenzi na kuondoka vifundo. Lakini wasipopeana mkono kabla ya swalah ya faradhi basi itasuniwa kupeana mikono baada yake baada ya Dhikr iliyowekwa katika Shari´ah.

Kuhusu yale yanayofanywa na baadhi ya watu ambapo wanaharakia kupeana mikono baada ya swalah ya faradhi punde tu baada ya kutoa salamu ya pili, sijui msingi wa kitu hicho. Bali udhahiri ni kuchukizwa kwa jambo hilo kwa sababu ya kutokuwa dalili ya hilo. Isitoshe kilichowekwa katika Shari´ah kwa mswaliji katika hali kama hii ni yeye kuharakisha kuleta Adhkaar zilizowekwa katika Shari´ah zilizokuwa zikifanywa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya kutoa salamu ya swalah ya faradhi.

Ama kuhusu swalah iliyopendekezwa imewekwa katika Shari´ah kupeana mikono baada ya kutoa Tasliym ikiwa hawakupeana mikono kabla ya kuanza kuswali. Itatosha kama walipeana mikono kabla ya hapo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 37-38
  • Imechapishwa: 24/08/2022