Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Ama baada ya hayo;

1 – Ni jambo limesuniwa kwa mfungaji kutumia Siwaak. Imependekezwa kwake kufanya hivo wakati wa kila swalah na wakati wa kila wudhuu´. Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyeeeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Lau isingelikuwa kuwatilia uzito Ummah wangu basi ningeliwaamrisha Siwaak pamoja na kila swalah.”[1]

Katika Hadiyth ya Zuhayr bin Harb iliyopokelewa na Muslim imekuja:

“Lau isingelikuwa kuwatilia uzito Ummah wangu basi ningeliwaamrisha Siwaak wakati wa kila swalah.”[2]

Ibn Khuzaymah amesema katika “as-Swahiyh” yake:

”Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliposema:

“Lau isingelikuwa kuwatilia uzito Ummah wangu basi ningeliwaamrisha Siwaak wakati wa kila swalah.”

hakupambanua ambaye hakufunga na aliyefunga. Ndani yake kuna dalili inayofahamisha ya kwamba mfungaji kutumia Siwaak wakati wa kila swalah kuna ubora kwake kama ilivyo kwa ambaye hakufunga.”[3]

at-Tirmidhiy, Abu Daawuud na Ahmad wamepokea kupitia kwa ´Ammaar bin Rabiy´ah aliyesema:

“Nilimwona Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mara nisizoweza kuzihesabu akipiga Siwaak ilihali amefunga.”[4]

Katika cheni ya wapokezi wake yupo ´Aaswim bin ´Ubaydillaah bin ´Aaswim bin ´Umar bin al-Khattwaab. al-Bukhaariy, Ibn Ma´iyn na wengineo wamemdhoofisha. Lakini hata hivo at-Tirmidhiy amesema:

“Wanazuoni ni wenye kulitendea kazi jambo hili. Hawaoni ubaya wowote kwa mfungaji kutumia Siwaak. Ni mamoja mwanzoni mwa mchana na mwishoni mwake.”[5]

Maoni sahihi ni kwamba imesuniwa kupiga Siwaak mwanzoni na mwishoni mwa mchana. Lakini kwa sharti Siwaak hiyo isiwe yenye kuumiza wala kutoa chembechembe zikaingia kooni mwake. Kadhalika mswaki usiwe mkali kwa njia ya kwamba ukaondosha fizi na wala kusiwe kitu kingine miongoni mwa vile vitu vinavyowekwa na watu [kwenye mswaki huo] ukaufanya ukawa na utamtam.

[1] al-Bukhaariy (887) na Muslim (252).

[2] al-Bukhaariy (1934) na tamko ni lake, an-Nasaa´iy ameipokea ikiwa na cheni yenye kuungana katika ”as-Sunan al-Kubraa” (3037) na Ahmad (9928).

[3] Tazama ”Swahiyh Ibn Khuzaymah” (2006).

[4] Abu Daawuud (2364), at-Tirmidhiy (725) na tamko ni lake.

[5] Tazama ”Sunan-ut-Tirmidhiy” (725).   

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Duruus fiy Ramadhwaan, uk. 51-52
  • Imechapishwa: 24/04/2023