Wanashuhudia ya kwamba Allaah (Ta´ala) anamwongoza katika dini Yake yule amtakaye na anampotosha yule amtakaye. Hana hoja yoyote dhidi Yake yule ambaye Allaah amempotosha. Wala hana udhuru wowote Kwake. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

قُلْ فَلِلَّـهِ الْحُجَّةُ الْبَالِغَةُ ۖ فَلَوْ شَاءَ لَهَدَاكُمْ أَجْمَعِينَ

”Sema: ”Basi ni Allaah pekee ndiye Mwenye hoja ya kukata; na Angelitaka angelikuongozeni nyote.””[1]

Amesema (Jalla wa ´Alaa):

وَلَوْ شِئْنَا لَآتَيْنَا كُلَّ نَفْسٍ هُدَاهَا وَلَـٰكِنْ حَقَّ الْقَوْلُ مِنِّي

“Na Tungelitaka, basi tungeliipa kila nafsi mwongozo wake, lakini imethibiti kauli kutoka Kwangu.”[2]

وَلَقَدْ ذَرَأْنَا لِجَهَنَّمَ كَثِيرًا مِّنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ

“Hakika Tumeumba Moto wa Jahannam kwa ajili ya wengi katika majini na watu.”[3]

Yeye (Subhaanah) amewaumba viumbe bila kuwahitaji, ambapo akawafanya ni makundi mawili: kundi moja ni lenye kustareheshwa kutokana na fadhilah Zake, kundi jingine ni la Motoni kutokana na uadilifu Wake. Ameamua kati yao wawepo wapotofu na waongofu, wenye furaha na wala maangamivu, walio karibu na rehema Zake na walio mbali na rehema Zake:

لَا يُسْأَلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْأَلُونَ

“Haulizwi kwa yale Anayoyafanya, lakini wao wataulizwa.”[4]

Amesema (Jalla wa ´Alaa):

أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ ۗ تَبَارَكَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

”Tanabahi! Ni Vyake pekee uumbaji na amri. Amebarikika Allaah, Mola wa walimwengu!”[5]

فَرِيقًا هَدَىٰ وَفَرِيقًا حَقَّ عَلَيْهِمُ الضَّلَالَةُ

”Kundi Ameliongoza na kundi jingine limethibitikiwa upotevu.”[6]

أُولَـٰئِكَ يَنَالُهُمْ نَصِيبُهُم مِّنَ الْكِتَابِ

”Hao itawafikia sehemu yao waliyoandikiwa.”[7]

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

”Bi maana ile furaha na kula maangamivu kulikokwishatangulia.”[8]

Abu Muhammad al-Makhladiy ametukhabarisha: Abul-´Abbaas as-Sarraaj ametukhabarisha: Yuusuf bin Muusa ametuhadithia: Jariyr ametukhabarisha, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Zayd bin Wahb, kutoka kwa ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh), aliyesema: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), mkweli na mwenye kusadikishwa, ametuhadithia:

“Hakika kila mmoja wenu hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arobaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu. Kisha huwa donge la damu kwa muda kama huo. Kisha huwa pande la nyama kwa muda kama huo. Kisha Allaah humtumia Malaika ambaye huamrishwa kuandika mambo manne; riziki yake, muda wake wa kuishi, matendo yake na kama atakuwa mtu muovu au mwema. Naapa kwa ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake! Hakika mmoja atafanya matendo ya watu wa Peponi kiasi ambacho kusibaki kati yake yeye na yenyewe [Pepo hiyo] isipokuwa dhiraa, yamuwahi yale aliyotanguliziwa kwenye kitabu ambapo afanye matendo ya watu wa Motoni na auingie. Hakika mmoja atafanya matendo ya watu wa Motoni kiasi ambacho kusibaki kati yake yeye na wenyewe [Moto huo] isipokuwa dhiraa, yamuwahi yale aliyotanguliziwa kwenye kitabu ambapo afanye matendo ya watu wa Motoni na aingie.”[9]

Abu Muhammad al-Makhladiy ametukhabarisha: Abul-´Abbaas as-Sarraaj ametukhabarisha: Ishaaq bin Ibraahiym al-Handhwaliy – naye ni Ibn Raahuuyah – ametuhadithia: ´Abdus-Swamad bin ´Abdil-Waarith ametukhabarisha: Hammaad bin Salamah ametuhadithia, kutoka kwa Hishaam bin ´Urwah, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa), aliyesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakika mtu atafanya matendo ya watu wa Peponi ilihali amekwishaandikwa kwenye kitabu kuwa ni katika watu wa Motoni. Punde kabla ya kufa afanye matendo ya watu wa Motoni, afe na kuingia Motoni. Hakika mtu atafanya matendo ya watu wa Motoni ilihali amekwishaandikwa kwenye kitabu kuwa ni katika watu wa Peponi. Punde kabla ya kufa afanye matendo ya watu wa Peponi, afe na kuingia Peponi.”[10]

[1] 6:149

[2] 32:13

[3] 7:179

[4] 21:23

[5] 7:54

[6] 7:29-30

[7] 7:37

[8] Jaamiy´-ul-Bayaan (12/410).

[9] al-Bukhaariy (6549) na Muslim (2643).

[10] Ahmad (6/107). al-Haythamiy amesema:

“Ameipokea Ahmad na Abu Ya´laa. Baadhi ya cheni zake za wapokezi zina wasimulizi Swahiyh.” (Majma´-uz-Zawaa’id (7/212))

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 280-283
  • Imechapishwa: 19/12/2023