al-Jahm anadai kuwa amepata Aayah nyingine ndani ya Kitabu cha Allaah inayojulisha kuwa Qur-aan ni kiumbe. Tulipomuuliza ni Aayah ipi, akajibu maneno Yake Allaah (Ta´ala):

إِنَّمَا الْمَسِيحُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ رَسُولُ اللَّـهِ وَكَلِمَتُهُ أَلْقَاهَا إِلَىٰ مَرْيَمَ وَرُوحٌ مِّنْهُ

”Hakika si vyenginevyo al-Masiyh ‘Iysaa, mwana wa Maryam, ni Mtume wa Allaah na ni neno Lake alompelekea Maryam na roho kutoka Kwake.”[1]

Anasema kuwa ´Iysaa (´alayhis-Salaam) ni kiumbe.

Kwa kweli Allaah amekunyima kuielewa Qur-aan. ´Iysaa amesifiwa kwa matamshi ambayo hayakusifiwa ndani ya Qur-aan. Amesifiwa (´alayhis-Salaam) mwenye kuzaliwa, mtoto na mvulana, anayekula na kunywa, ambaye amezungumzishwa kuamrishwa na kukatazwa, kuzungumzishwa, kuahidiwa na kutishiwa. Isitoshe ni miongoni mwa kizazi cha Nuuh na miongoni mwa kizazi cha Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haijuzu kwetu kusema juu ya Qur-aan yale tunayosema juu ya ´Iysaa. Mmemsikia Allaah akisema juu ya Qur-aan aliyoyasema kuhusu ´Iysaa?

Kuhusu Aayah:

إِنَّمَا الْمَسِيحُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ رَسُولُ اللَّـهِ وَكَلِمَتُهُ أَلْقَاهَا إِلَىٰ مَرْيَمَ وَرُوحٌ مِّنْهُ

”Hakika si vyenginevyo al-Masiyh ‘Iysaa, mwana wa Maryam, ni Mtume wa Allaah na ni neno Lake alompelekea Maryam na roho kutoka Kwake.”

inahusu lile neno ambalo Maryam alishika ujauzito kwalo, nalo ni ”Kuwa!” Kwa hiyo ´Iysaa (´alayhis-Salaam) akawa kwa neno ”Kuwa!”. Si kwamba ´Iysaa yeye ndiye ”Kuwa!”, lakini amekuwa kupitia neno ”Kuwa!”. Neno hili limetoka kwa Allaah na si kiumbe.

Manaswara na Jahmiyyah wamemsemea uwongo Allaah inapokuja kwa ´Iysaa (´alayhis-Salaam). Jahmiyyah wanadai kuwa ´Iysaa ni roho ya Allaah na neno Lake, kwa sababu neno ni kiumbe. Manaswara wanadai kuwa ni roho ya Allaah na anatokana na dhati ya Allaah, ni kama ambavo mtu husema kuwa kitambaa hiki kinatokana na vazi hili. Sisi tunasema kuwa ´Iysaa amekuwa kwa neno ”Kuwa!”, na si kwamba yeye ndiye neno. Ama kuhusu:

وَرُوحٌ مِّنْهُ

”… na roho kutoka Kwake.”

Bi maana amekuwa (´alayhis-Salaam) kutokana na amri Yake. Kama alivosema (Ta´ala):

وَسَخَّرَ لَكُم مَّا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا مِّنْهُ

”Amekutiishieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini vyote humo.”[2]

Bi maana kutokana na amri Yake. Roho ya Allaah tafsiri yake ni roho iliyoumbwa kwa neno la Allaah. Ni kama inavosemwa mja wa Allaah, mbingu ya Allaah na ardhi ya Allaah[3].

[1] 4:171

[2] 45:13

[3] Ibn ´Aqiyl al-Hanbaliy amesema:

”Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ameandika kitabu kinachoitwa ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah wal-Qadariyyah.” (al-Aadaab ash-Shar´iyyah (1/274))

Ibn Taymiyyah amesema:

”Kama alivosema Imaam Ahmad katika kitabu chake ”ar-Radd ´alaaz-Zanaadiqah wal-Jahmiyyah.”  (Tafsiyr Suurat-il-Ikhlaasw, uk. 239)

Ibn Kathiyr amesema:

”… na hivo ndivo alivosema Ahmad bin Hanbal katika kitabu ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah” (Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (3/304))

Ibn Hajar al-´Asqalaaniy amesema:

”Amesema waziwazi Ahmad katika kitabu “ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah.” (Fath-ul-Baariy (13/598))

  • Mhusika: Imaam Ahmad bin Hanbal (afk. 241)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 125-127
  • Imechapishwa: 23/04/2024