Isitoshe al-Jahm anasema kuwa yeye anayo dalili nyingine ndani ya Kitabu cha Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) inayofahamisha kuwa Qur-aan ni kiumbe. Tunapouliza ni Aayah ipi hiyo, anajibu:

مَا يَأْتِيهِم مِّن ذِكْرٍ مِّن رَّبِّهِم مُّحْدَثٍ

“Hakuna ukumbusho wowote ule mpya unaowajia kutoka kwa Mola wao… “[1]

Akadai kuwa Allaah anasema kuwa Qur-aan imezuka – na kila chenye kuzuka kimeumbwa! Namna hii ndivo anaeneza hoja zake tata kwa watu. Ni miongoni mwa zile Aayah zenye kutatiza. Nikazungumzia suala hilo, nikamtaka msaada Allaah na nikakitazama Kitabu cha Allaah – hapana uwezo wa kutikisika wala namna isipokuwa kwa msaada wa Allaah.

Wakati mambo mawili yanaposhirikiana majina, ambapo kimoja wapo kikawa juu zaidi kuliko kingine, na yote mawili yametajwa katika mazingira ya kusifiwa, basi sifa hizo zinakuwa kwa kile kilicho juu zaidi kuliko kile kilicho chini. Na ikiwa yametajwa katika mazingira ya masimango, basi masimango hayo yanakuwa kwa kile kilicho chini zaidi kuliko kile kilicho juu. Kwa mfano Allaah (Ta´ala) anasema ndani ya Kitabu Chake:

إِنَّ اللَّـهَ بِالنَّاسِ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Hakika Allaah kwa watu ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[2]

عَيْنًا يَشْرَبُ بِهَا عِبَادُ اللَّـهِ يُفَجِّرُونَهَا تَفْجِيرًا

”Nayo ni chemchem watakayokunywa humo Waja wa Allaah, wataitumia kuipitisha wanavyotaka mapitisho mazuri.”[3]

Bi maana wale wema pasi na wale waovu. Ilipokuwa makundi yote mawili yamekusanya watu na waja, basi walengwa katika Aayah:

عَيْنًا يَشْرَبُ بِهَا عِبَادُ اللَّـهِ يُفَجِّرُونَهَا تَفْجِيرًا

”Nayo ni chemchem watakayokunywa humo Waja wa Allaah, wataitumia kuipitisha wanavyotaka mapitisho mazuri.”

Kwa sababu Amewasema (Ta´ala) wale wema kwa kuwapwekesha:

إِنَّ الْأَبْرَارَ لَفِي نَعِيمٍ

“Hakika waumini watendao mema kwa wingi bila shaka watakuwa katika neema… ”[4]

Na Akasema wale waovu kwa kuwapwekesha:

وَإِنَّ الْفُجَّارَ لَفِي جَحِيمٍ

”… na hakika watendao dhambi bila shaka watakuwa katika Moto uwakao vikali mno.”[5]

Vivyo hivyo Aayah isemayo:

وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا

“… Naye ni Mwenye kuwarehemu waumini.”[6]

Waumini ndio wana haki zaidi ya mkabala huo hata kama Aayah inawazungumzia watu. Kwa sababu muumini anapotajwa peke yake, anatajwa kwa lengo la kusifiwa:

إِنَّ اللَّـهَ بِالنَّاسِ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“Hakika Allaah kwa watu ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”

وَكَانَ بِالْمُؤْمِنِينَ رَحِيمًا

“… Naye ni Mwenye kuwarehemu waumini.”[7]

Na wakati makafiri wanapotajwa peke yao, wanachukua sehemu ya masimango katika maneno Yake (Ta´ala):

أَلَا لَعْنَةُ اللَّـهِ عَلَى الظَّالِمِينَ

”Zinduka! Laana ya Allaah iko juu ya waliodhulumu.”[8]

أَن سَخِطَ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ وَفِي الْعَذَابِ هُمْ خَالِدُونَ

”… kwamba Allaah amewakasirikia na katika adhabu wao watadumu.”[9]

Watu hawa hawaingii ndani ya rehema.

Amesema (Ta´ala):

وَلَوْ بَسَطَ اللَّـهُ الرِّزْقَ لِعِبَادِهِ لَبَغَوْا فِي الْأَرْضِ

”Na lau kama Allaah angelikunjua riziki kwa Waja Wake, basi wangevuka mipaka katika ardhi.”[10]

Jina la waja limekusanya makafiri na waumini wote, pamoja na hivyo kafiri ana wepesi zaidi ya kuchupa mipaka kuliko muumini, kwa sababu waumini wamesifiwa pale walipotajwa peke yao katika mazingira kama hayohayo, nayo:

وَالَّذِينَ إِذَا أَنفَقُوا لَمْ يُسْرِفُوا وَلَمْ يَقْتُرُوا وَكَانَ بَيْنَ ذَٰلِكَ قَوَامً

“Na wale ambao wanapotoa huwa hawafanyi israfu na wala hawafanyi uchoyo na wanakuwa wastani baina ya hayo.”[11]

وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ

”… na hutoa sehemu katika vile tulivyowaruzuku.”[12]

Allaah alimkunjulia riziki Sulaymaan bin Daawuud, Dhul-Qarnayn, Abu Bakr, ´Umar na mfano wao na hawakuchupa mipaka. Wakati makafiri wanapotajwa peke yao, kuchupa mipaka kunakuwa kwao. Amesema (Ta´ala) kuhusu Qaaruun:

إِنَّ قَارُونَ كَانَ مِن قَوْمِ مُوسَىٰ فَبَغَىٰ عَلَيْهِمْ

”Hakika Qaaruun alikuwa miongoni mwa watu wa jamii ya Muusa, lakini akachupa mpaka katika kuwafanyia kiburi.”[13]

Vivyo hivyo kuhusu Namruud bin Kan´aan, ambaye Allaah alimpa ufalme na baadaye akahoji juu ya Mola Wake. Mfano wa hayo pia yanaweza kusemwa juu ya Fir´awn. Muusa (´alayhis-Salaam) alisema juu yake:

رَبَّنَا إِنَّكَ آتَيْتَ فِرْعَوْنَ وَمَلَأَهُ زِينَةً وَأَمْوَالًا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا

”Ee Mola Wetu! Hakika Wewe umempa Fir´awn na wakuu wake mapambo na mali katika uhai wa dunia.”[14]

Kwa hivyo pindi wote wawili walipotajwa katika mazingira hayohayo, ya kuchupa mipaka, basi ikawa inawahusu zaidi makafiri. Upande mwingine waumini wanahusika zaidi katika mazingira ya kusifiwa. Vivyo hivyo kuhusu Aayah:

مَا يَأْتِيهِم مِّن ذِكْرٍ مِّن رَّبِّهِم مُّحْدَثٍ

“Hakuna ukumbusho wowote ule mpya unaowajia kutoka kwa Mola wao… “

Hapa amekusanya makumbusho mawili: ukumbusho wa Allaah na ukumbusho wa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Pindi kunapotajwa ukumbusho wa Allaah peke yake, basi si wenye kuzuka. Hukumsikia akisema:

وَلَذِكْرُ اللَّـهِ أَكْبَرُ

”Na hakika kumtaja Allaah ndio kukubwa zaidi.”[15]

وَهَـٰذَا ذِكْرٌ مُّبَارَكٌ أَنزَلْنَاهُ

”Huu ni ukumbusho uliobarikiwa Tumeuteremsha? [16]

Wakati ukumbusho wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) unapotajwa peke yake, basi  ni wenye kuzuka. Hukumsikia akisema:

وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ

“Allaah amekuumbeni pamoja na vile mnavovifanya?”[17]

Ukumbusho wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) umetanguliwa na kitendo, na Allaah ndiye ambaye kauumba na kuufanya uzuke. Dalili ya makumbusho haya mawili ni maneno Yake:

مَا يَأْتِيهِم مِّن ذِكْرٍ مِّن رَّبِّهِم مُّحْدَثٍ

“Hakuna ukumbusho wowote ule mpya unaowajia kutoka kwa Mola wao… “[18]

Amesema kuwa ni mpya pale wakati ulipotujia. Unajua kuwa hakuna aliyetuletea nayo isipokuwa mfikishaji na mkumbushaji. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَذَكِّرْ فَإِنَّ الذِّكْرَىٰ تَنفَعُ الْمُؤْمِنِينَ

“Na kumbusha; kwani hakika ukumbusho [mawaidha] unawafaa waumini.”

فَذَكِّرْ إِن نَّفَعَتِ الذِّكْرَىٰ

“Basi kumbusha ikiwa kunafaa ukumbusho.”[19]

فَذَكِّرْ إِنَّمَا أَنتَ مُذَكِّرٌ

”Basi kumbusha! Hakika mambo yalivyo wewe ni mkumbushaji tu.”[20]

Wakati yalipokusanyikiwa neno ukumbusho, ndipo ikatumika neno hilohilo la uzukaji. Wakati ukumbusho wa Mtume (Swalla Allaahu ´aalyhi wa sallam) unapotajwa kwa kupwekeka, basi unaingiliwa na jambo la uumbaji na uzukaji. Lakini mambo sivyo inapokuja katika ukumbusho wa Allaah, ambao haungiliwi na jambo la uumbaji wala uzukaji. Kwa hivyo tunapata kufahamu ya kwamba maneno Yake (Ta´ala):

مَا يَأْتِيهِم مِّن ذِكْرٍ مِّن رَّبِّهِم مُّحْدَثٍ

“Hakuna ukumbusho wowote ule mpya unaowajia kutoka kwa Mola wao… “

analengwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hajui, ambapo Allaah akamfunza. Pindi Allaah alipomfunza, basi elimu hiyo ikawa ni kitu kilichozuka kwake yeye Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[21].

[1] 21:2

[2] 22:65

[3] 76:6

[4] 82:13

[5] 82:14

[6] 33:43

[7] 33:43

[8] 11:18

[9] 5:80

[10] 42:27

[11] 25:67

[12] 2:3

[13] 28:76

[14] 10:88

[15] 29:45

[16] 21:50

[17] 37:96

[18] 21:2

[19] 87:9

[20] 88:21

[21] Ibn ´Aqiyl al-Hanbaliy amesema:

”Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ameandika kitabu kinachoitwa ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah wal-Qadariyyah.” (al-Aadaab ash-Shar´iyyah (1/274))

Ibn Taymiyyah amesema:

”Kama alivosema Imaam Ahmad katika kitabu chake ”ar-Radd ´alaaz-Zanaadiqah wal-Jahmiyyah.”  (Tafsiyr Suurat-il-Ikhlaasw, uk. 239)

Ibn Kathiyr amesema:

”… na hivo ndivo alivosema Ahmad bin Hanbal katika kitabu ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah” (Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (3/304))

Ibn Hajar al-´Asqalaaniy amesema:

”Amesema waziwazi Ahmad katika kitabu “ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah.” (Fath-ul-Baariy (13/598))

  • Mhusika: Imaam Ahmad bin Hanbal (afk. 241)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 120-125
  • Imechapishwa: 23/04/2024