Miongoni mwa mambo yanayojulisha elimu yenye manufaa ni kwamba mwenye nayo hajidai elimu na hajifakhari nayo juu ya yeyote. Hawatii wengine ujingani isipokuwa wale wanaokwenda kinyume na Sunnah na Ahl-us-Sunnah; watu kama hawa anawasema vibaya kutokana na ghadhabu zake kwa ajili ya Allaah, na si kutokana na nafsi yake wala kutaka kujikwaza juu ya yeyote.

Yule ambaye elimu yake si yenye manufaa hana shughuli nyingine isipokuwa kufanya kiburi kutokana na elimu yake juu ya watu, kuonyesha ubora wa elimu yake juu yao, kuwatia ujingani na kuwaponda ili apate kuwa juu yao. Mwenendo kama huu ni katika sifa mbaya na mbovu kabisa. Pengine hata akawanasibishia ujinga, ughafilikaji na usahaulifu wale wanazuoni waliotangulia. Hivyo hilo likampelekea kuwa mbinafsi, kutafuta umaarufu na kujidhania vizuri mwenyewe, na sambamba na hilo akawadhania vibaya wale waliotangulia.

Watu walio na elimu yenye manufaa wako kinyume na mwenendo huo. Wanazijengea dhana mbaya nafsi zao na wanawajengea dhana nzuri wanazuoni waliotangulia. Wanakiri kwa mioyo na nafsi zao ubora wa wale waliotangulia juu yao na kukubali kwamba hawawezi hata kukurubia ngazi za wale waliotangulia, sembuse kuzifikia ngazi zao. Ni uzuri ulioje wa maneno ya Abu Haniyfah wakati alipoulizwa ni nani mbora kati ya ´Alqamah na al-Aswad:

“Naapa kwa Allaah! Mimi siko katika ngazi yao mpaka niwataje; seuze kumfadhilisha yeyote kati yao.”

Ibn-ul-Mubaarak alipokuwa akitaja tabia za Salaf basi husoma mashairi:

Usitutaje sisi sambamba na wao

mzima hatembei kama mwenye kuchechemea

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Fadhwl ´Ilm-is-Salaf ´alaa ´Ilm-il-Khalaf, uk. 83-84
  • Imechapishwa: 29/09/2021