Je, talaka daima inakuwa ni shari na yenye kuchukiza? Hapana. Wakati mwingine hali inaweza kufikia kulazimika kuitoa ikihitajia. Wakati fulani haisilihi hali ya wanandoa isipokuwa kuachana baada ya kuwa wamejaribu kila njia kuleta suluhu lakini ikashindikana kumaliza magomvi.

Ibn Taymiyyah amesema:

”Allaah (Ta´ala) amemuhalalishia mwanaume talaka kama vile watu wanavyohitajia kile kilichoharamishwa kutokana na haja.”[1]

Miongoni mwa dalili za kuhalalishwa talaka mtu akihitajia ni maneno Yake (Ta´ala):

وَإِنْ عَزَمُوا الطَّلَاقَ فَإِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ

”Wakiazimia talaka, basi hakika Allaah ni Msikivu wa kila kitu, Mjuzi wa yote.”[2]

وَإِن يَتَفَرَّقَا يُغْنِ اللَّـهُ كُلًّا مِّن سَعَتِهِ ۚ وَكَانَ اللَّـهُ وَاسِعًا حَكِيمًا

“Wakifarikiana basi Allaah atampa utajiri kila mmoja katika wasaa Wake; na Allaah ni Mwenye wasaa, Mwenye hekima.”[3]

Ibn Kathiyr amesema katika ”Tafsiyr” yake:

”Allaah (Ta´ala) amesimulia ya kwamba wakiachana, basi Allaah atamtosheleza mwanaume kutokana na mwanamke huyo na mwanamke atamtosheleza kutokana na mwanaume huyo kwa njia ya kwamba Allaah atampa badala mwanaume kwa ambaye ni mbora kuliko mwanamke huyo na pia atampa badala mwanamke kwa ambaye ni mbora kuliko mwanaume huyo.”[4]

Imepokelewa katika Hadiyth kupitia kwa Ibn ´Abbaas ambaye amesimulia:

”Mke wa Thaabit alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema: ”Naapa kwa Allaah! Simtii kasoro yoyote ya tabia wala dini, hata hivyo nachukia ukafiri baada ya Uislamu.”Akamwambia: ”Je, utamrudishia shamba lake?” Akajibu: ”Ndio.” Ndipo akasema: ”Ee Thaabit, kubali shamba kisha umtaliki.”[5]

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, jamaa zake na Maswahabah zake wote.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (33/21).

[2] 02:227

[3] 04:130

[4] Tafsiyr Ibn Kathiyr (02/431).

[5] al-Bukhaariy (5673).

  • Mhusika: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Twalaaq – asbaabuhu wa ´ilaajuh, uk. 51-53
  • Imechapishwa: 30/04/2024