Imaam Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah) amesema:

Amesema (Ta´ala) kuhusu makafiri:

وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ

”Na Allaah awaghadhibikie.”[1]

MAELEZO

7 – Kughadhibika. Kughadhibika ni miongoni mwa sifa za Allaah zilizothibiti kwa Qur-aan, Sunnah na maafikiano ya Salaf. Allaah (Ta´ala) amesema juu ya mwenye kumuua muumini kwa makusudi:

وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَلَعَنَهُ

“Na Allaah atamghadhibikia na atamlaani.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah ameandika kitabu huko Kwake juu ya ´Arshi “Hakika rehema Zangu zinashinda ghadhabu Zangu.””[3]

Kuna maafikiano juu yake.

Salaf wameafikiana juu ya kuthibitisha Allaah (Ta´ala) kughadhabika. Kwa hiyo ni lazima kumthibitishia nayo pasi na kupotosha, kukanusha, kuifanyia namna wala kuipigia mfano. Ni kughadhibika kikweli ambako kunalingana na Allaah (Ta´ala).

Ahl-ut-Ta´twiyl wameifasiri kuwa ni kulipiza kisasi. Tunawaraddi kwa yale yaliyokwishatangulia katika kanuni ya nne. Kuna njia nyingine ya nne ambayo; Allaah ametofautisha kati ya kughadhibika na kulipiza kisasi. Amesema (Ta´ala):

فَلَمَّا آسَفُونَا

”Basi walipotukasirisha… “

Bi maana pindi walipotukasirisha.

انتَقَمْنَا مِنْهُمْ

“… Tuliwapatiliza.”[4]

Akafanya kulipiza kisasi ni natija ya ghadhabu. Kwa hiyo ni dalili kuwa ni mambo mawili tofauti.

Amesema (Ta´ala):

اتَّبَعُوا مَا أَسْخَطَ اللَّـه

“… wao wamefuata yale yanayomghadhibisha Allaah.”[5]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah anachukia kwenu mambo matatu; porojo, kuharibu mali na kuulizauliza na kuombaomba.”[6]

Ameipokea al-Bukhaariy.

Salaf wameafikiana juu ya kumthibitishia Allaah jambo hilo. Kwa hiyo ni lazima kumthibitishia nayo kikweli pasi na kupotosha, kukanusha, kuifanyia namna wala kuipigia mfano. Ni kuchukia kwa Allaah kikweli ambako kunalingana Naye.

Ahl-ut-Ta´twiyl wamefasiri kuwa ni kutengwa mbali. Tunawaraddi kwa yale yaliyokwishatangulia katika kanuni ya nne.

[1] 48:06

[2] 04:93

[3] al-Bukhaariy (7554) na Muslim (2751).

[4] 43:55

[5] 47:28

[6] al-Bukhaariy (5975) na Muslim (593).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 55-57
  • Imechapishwa: 20/10/2022