31. Sifa na majina ya Allaah yaliyothibiti katika Sunnah I

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio yenye kuifasiri Qur-aan na kuiweka wazi, kuithibitisha na kuja na maana mpya na hukumu [ambazo hazikuja katika Qur-aan]. Vilevile ni wajibu kuamini yale Mtume aliyomsifu kwayo Mola Wake (´Azza wa Jall) kutokana na zile Hadiyth Swahiyh ambazo wamezikubali watu wa maarifa, kwa mfano maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Huteremka Mola Wetu katika mbingu ya dunia kila usiku pale kunapobaki theluthi ya mwisho ya usiku na Kusema: “Ni nani mwenye kuniomba nimjibie? Ni nani mwenye kuniuliza nimpe? Ni nani mwenye kuniomba msamaha nimsamehe?”[1]

“Allaah Hufurahi sana kwa Tawbah ya mja Wake muumini anapotubia, kuliko furaha ya mmoja wenu kwa kupata kipando chake… ”[2]

“Allaah Anawacheka watu wawili ambapo mmoja wao kamuua mwenzake. Halafu wote wawili wanaingia Peponi.”[3]

“Anastaajabu Mola Wetu kwa kukata tamaa waja Wake licha ya mabadiliko Yake ya hali zao yako karibu. Huwatazama mnapokuwa katika hali ngumu na wenye kukata tamaa. Huanza kucheka kwa kuwa Anajua kuwa faraja yenu iko karibu.”[4]

“Haitoacha Jahannam kutupwa ndani yake [watu na mawe] nayo inasema “Je, kuna zaidi?”, mpaka Mola Aliyetukuka Aweke Mguu Wake kisha pawe sawa. Hapo ndio itasema ­­“Inatosha! Inatosha!”[5]

“Allaah (Ta´ala) Atasema: “Ee Aadam!” Atajibu: “Ninaitikia wito Wako na nakuomba unifanye ni mwenye furaha na Kunisaidia.” Kisha Atanadi kwa Sauti: “Hakika Allaah Anakuamrisha utoe moja katika kizazi chako Motoni.””[6]

MAELEZO

Hadiyth hizi sita ni kama Aayah zilizo kabla yake. Ni kama jinsi Qur-aan inavyofahamisha kuthibitisha sifa na majina kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kwamba Yeye (Jalla wa ´Alaa) anaitwa kwa majina mazuri kabisa na anasifika vilevile kwa sifa kuu. Kama ambavyo imekuja katika Qur-aan kadhalika imekuja katika Sunnah.

Hakika ya Sunnah Swahiyh za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zinaifasiri Qur-aan, kuibainisha, kuithibitisha na kuja na maana na hukumu mpya. Qur-aan imetoa ushahidi juu ya hili. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ

“Hakika waumini [wa kweli] ni wale waliomwamini Allaah na Mtume Wake… ” (24:62)

أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ

“Mtiini Allaah na mtiini Mtume.” (04:59)

وَالنَّجْمِ إِذَا هَوَىٰ مَا ضَلَّ صَاحِبُكُمْ وَمَا غَوَىٰ وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ

“Naapa kwa nyota inapotua. Hakupotea sahibu yenu na wala hakukosea. Na wala hatamki kwa matamanio yake. Hayo [ayasemayo] si chochote isipokuwa ni Wahy unaofunuliwa.” (53:01-04)

Kama ambavyo kumekuja Aayah zenye kuzungumzia sifa na majina ya Allaah na Sunnah imefanya vivyo hivyo. Yaliyothibiti katika Sunnah Swahiyh hukumu yake ni kama ile iliyothibiti katika Qur-aan. Kwa hivyo itakuwa ni wajibu kumthibitishia nayo Allaah na kuamini kuwa ni sifa na majina ya Allaah kwa njia inayolingana Naye (Subhaanah) pasi na kupotosha, kukanusha, kuzifanyia namna na kulinganisha. Mlango na hukumu ni moja. Yaliyokuja katika Sunnah Swahiyh hukumu yake ni kama yaliyokuja katika Qur-aan. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaonelea kuwa yote ni sawa sawa. Kwa mfano maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

Dalili ya kwamba Allaah Huteremka katika mbingu ya chini

“Huteremka Mola Wetu katika mbingu ya dunia kila usiku pale kunapobaki theluthi ya mwisho ya usiku na Kusema: “Ni nani mwenye kuniomba nimjibie? Ni nani mwenye kuniuliza nimpe? Ni nani mwenye kuniomba msamaha nimsamehe?”

Ahl-us-Sunnah wanamthibitishia Allaah sifa ya ushukaji huu. Ni ushukaji unaolingana na Allaah. Hafanani na viumbe Wake katika ushakaji Wake. Kiumbe yeye kwa mfano hushuka kutoka juu na kwenda chini na kutoka juu ya mlima na kwenda chini. Lakini hata hivyo ushukaji wa Allaah sio kama ushukaji wa kiumbe. Kadhalika neno la Allaah sio kama neno la kiumbe, wito wa Allaah sio kama wito wa kiumbe na maneno ya Allaah sio kama maneno ya kiumbe. Sifa za Allaah ni zenye kulingana Naye na Yeye ndiye Mwenye kumuitikia muombaji:

“Ni nani mwenye kuniomba nimjibie? Ni nani mwenye kuniuliza nimpe? Ni nani mwenye kuniomba msamaha nimsamehe?”

Hakika Yeye ni Mwingi wa kutoa na ni Mkarimu (Subhaanahu wa Ta´ala). Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu. Ni wajibu kumthibitishia Allaah sifa hizi kwa njia inayolingana Naye. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

Dalili ya Kucheka kwa Allaah

“Allaah Anawacheka watu wawili ambapo mmoja wao kamuua mwenzake. Halafu wote wawili wanaingia Peponi.”

Ni kucheka kunakolingana na Allaah. Hashabihiani na viumbe Vyake katika sifa zao na kucheka kwao. Bali sifa za Allaah zinalingana Naye na zinahusiana Naye (Jalla wa ´Alaa). Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

Dalili ya Kustaajabu kwa Allaah

“Anastaajabu Mola Wetu kwa kukata tamaa waja Wake licha ya mabadiliko Yake ya hali zao yako karibu… “

Bi maana mambo kubadilika. Mtu wakati mwingine anaweza kukata tamaa kutokana na njaa kali pamoja na kuwa faraja ya Allaah iko karibu.

“… Huwatazama mnapokuwa katika hali ngumu na wenye kukata tamaa. Huanza kucheka kwa kuwa Anajua kuwa faraja yenu iko karibu.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

Dalili kuwa maneno ya Allaah ni ya Herufi na Sauti

“Allaah (Ta´ala) Atasema: “Ee Aadam!” Atajibu: “Ninaitikia wito Wako na nakuomba unifanye ni mwenye furaha na Kunisaidia.” Kisha Atanadi kwa Sauti: “Hakika Allaah Anakuamrisha utoe moja katika kizazi chako Motoni.””

Hapa kuna uthibitisho wa sauti kwa Allaah na kwamba Yeye (Subhaanah) ana sauti yenye kusikika. Sauti hiyo waliisikia Malaika, Muusa (´alayhis-Salaam) na aliisikia vilevile Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) usiku wa Israa´.

Maneno Yake (Ta´ala):

“Hakika Allaah Anakuamrisha utoe moja katika kizazi chako Motoni.”

Imekuja katika Hadiyth nyingine:

“Miongoni mwa [watu] elfu moja [kutabaki] mia tisa tisini na tisa.”

Idadi hii ndio itatolewa Motoni. Hakuna atayeokoka katika idadi elfu moja isipokuwa mtu mmoja tu na mia tisa tisini na tisa watabakizwa Motoni. Hii inaonyesha ni khatari kubwa iliyoje itakuwepo. Kwa ajili hii ndio maana (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَمَا أَكْثَرُ النَّاسِ وَلَوْ حَرَصْتَ بِمُؤْمِنِينَ

Na wengi wa watu hawatoamini japokuwa utatilia hima.” (12:103)

وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ

“Na kama ukiwatii wengi walioko ulimwenguni, watakupoteza na njia ya Allaah.” (06:116)

وَلَقَدْ صَدَّقَ عَلَيْهِمْ إِبْلِيسُ ظَنَّهُ

“Na kwa yakini Ibliys alisadikisha dhana yake juu yao.” (34:20)

Pindi Maswahabah waliposikia kuhusu jambo hili ya kwamba katika watu elfu moja kutatolewa mmoja, jambo hili liliwawia zito kwao. Ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaambia katika ukamilifu wa Hadiyth:

“Msikhofu! Hawa mia tisa tisini na tisa ni katika Ya´juu na Ma´juuj. Miongoni mwenu kuna mmoja tu katika Ummah wa Muhammad mbali na Ya´juuj Na Ma´juuj.”

Hii ni dalili yenye kuonyesha kuwa wengi wataoingia Motoni ni katika Ya´juuj na Ma´juuj. Hawa ni watu waovu kabisa ambao watajitokeza katika zama za mwisho. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa salla):

Dalili ya Mguu wa Allaah

“Haitoacha Jahannam kutupwa ndani yake [watu na mawe] nayo inasema “Je, kuna zaidi?”, mpaka al-Jabbaar aweke ndani yake Mguu Wake.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… Mguu Wake kisha pawe sawa. Hapo ndio itasema ­­“Inatosha! Inatosha!”[7]

Hapa kuna uthibitisho wa mguu. Inatakiwa kuthibitisha mguu kwa njia inayolingana na Allaah. Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona, ana mkono na mguu. Zote hizi ni sifa zinazolingana Naye. Hashabihiani na viumbe katika sifa Zake. Hafanani nao katika usikizi Wake, uoni Wake, mkono Wake, mguu Wake, kucheka Kwake na nyenginezo. Kucheka kwa Allaah na kusikia Kwake kunalingana Naye na upande mwingine sifa za viumbe zinalingana nao. Amesema (Ta´ala):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)
 

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

 
  “Na wala hana yeyote anayefanana [kulingana] Naye.” (112:04)  

فَلَا تَضْرِبُوا لِلَّـهِ الْأَمْثَالَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

 
”Basi msipigie mifano Allaah! Hakika Allaah Anajua nanyi hamjui.”(16:74)  

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanasema namna hii kuhusu sifa zote. Mlango wake ni mmoja. Hili ni tofauti na Jahmiyyah, Mu´tazilah, Ashaa´irah na wengineo walioziharibu sifa za Allaah. Jahmiyyah wanakanusha majina na sifa za Allaah vyote viwili. Mu´tazilah wanakanusha sifa na wakati huo huo wamethibitisha majina matupu yasiyokuwa na maana. Ashaa´irah na mapote mengine wamekanusha baadhi na wakati huo huo wakathibitisha nyenginezo.

Usawa ni kuthibitisha majina na sifa zote za Allaah zilizokuja katika Qur-aan na Sunnah. Yale sahihi yaliyopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kama mfano wa yale yaliyokuja katika Qur-aan. Ni wajibu kumthibitishia nayo Allaah kwa njia inayolingana Naye bila ya kupotosha, kukanusha, kuzifanyia namna na kulinganisha. Inatakiwa kuyathibitisha katika mpaka wa Kauli Yake (Subhaanah):

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)
 

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

 
  “Na wala hana yeyote anayefanana [kulingana] Naye.” (112:04)

فَلَا تَضْرِبُوا لِلَّـهِ الْأَمْثَالَ

“Basi msimpigie mifano!” (16:74)

 

Vilevile Hadiyth isemayo:

Dalili ya Kufurahi kwa Allaah

“Allaah Hufurahi sana kwa Tawbah ya mja Wake muumini anapotubia, kuliko furaha ya mmoja wenu kwa kupata kipando chake… ”

Kufurahi kwa Allaah kunalingana na Allaah. Anafurahi lakini hata hivyo sio kama wanavyofurahi viumbe. Anaridhia lakini lakini sio kama wanavyoridhia viumbe. Anakasirika lakini lakini sio kama wanavyokasirika viumbe.

Hadiyth hii inahusiana na mtu aliyempoteza ngamia wake na alikuwa jangwani amelala chini ya mti na huku anasubiri tu mauti yamfike. Tahamaki akamuona ngamia wake amesimama juu ya kichwa chake. Akasema kutokana na wingi wa furaha:

“Ee Allaah! Hakika wewe ni mja wangu na mimi ndiye Mola Wako.” Alikosea kutokana na wingi wa furaha.””

Allaah (Subhaanah) ni mwenye furaha zaidi juu ya tawbah ya mja Wake kuliko mtu huyu. Pamoja na kuwa Yeye ndiye ambaye amemtunukia tawbah hii. Lakini pamoja na hivyo anaifurahia kutoka kwa mja Wake. Allaah (Jalla wa ´Alaa) ndiye ambaye amemtunukia na kumuwafikisha nayo.

[1] al-Bukhaariy (7494) na Muslim (758).

[2] al-Bukhaariy (6308) na (2744).

[3] al-Bukhaariy (2826) na Muslim (1890).

[4] Ahmad (4/11) na Ibn Maajah (181). Katika mlolongo wa wapoezi wake kuna udhaifu. Katika mlolongo wa wapokezi wake amekuja Wakiy´ bin Hadas. Imaam al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema kuwa ni mdhaifu katika ”Sunan Ibn Maajah”. Hata hivyo Hadiyth iliyopokelewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh): ”Allaah (´Azza wa Jalla) Hustaajabu kwa huyu na huyu… ” ni Swahiyh. Tazama “Swahiyh al-Bukhaariy” (4889)).

[5] al-Bukhaariy (4850) na Muslim (2846).

[6] al-Bukhaariy (3348) na Muslim (222).

[7] al-Bukhaariy (4850) na Muslim (2846).

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com