30. Sifa na majina ya Allaah yaliyothibiti katika Qur-aan VIII

Amesema (Ta´ala):

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

”[Kuna] nyuso siku hiyo zitanawiri. Zikimtazama Mola wake.” (75:22-23)

عَلَى الْأَرَائِكِ يَنظُرُونَ

”Kwenye makochi [ya fakhari] wakitazama.” (83:23)

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ

”Kwa wale waliofanya wema watapata [jazaa ya] Pepo na zaidi.” (10:26)

لَهُم مَّا يَشَاءُونَ فِيهَا وَلَدَيْنَا مَزِيدٌ

”Watapata humo wayatakayo na Kwetu kuna yaliyo ziada.” (50:35)

Mlango huu umekuja katika Kitabu cha Allaah (Ta´ala) sehemu nyingi. Yule mwenye kuizingatia Qur-aan na huku anatafuta uongofu wake, basi itambainikia Njia ya haki.

MAELEZO

Amesema (Jalla wa ´Alaa):

Dalili kwamba waumini watamuona Mola wao Aakhirah

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ

”[Kuna] nyuso siku hiyo zitanawiri.” (75:22)

Nyuso zitanawiri na kung´ara.

إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

Zikimtazama Mola wake.” (75:23)

Zitamtazama.

عَلَى الْأَرَائِكِ يَنظُرُونَ

”Kwenye makochi [ya fakhari] wakitazama.” (83:23)

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ

”Kwa wale waliofanya wema watapata [jazaa ya] Pepo na zaidi.” (10:26)

Neno “ziada” maana yake ni kuangalia uso wa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Yote haya ni haki. Hakika Yeye (Subhaanah) atawatazama waja Wake na wao watamtazama siku ya Qiyaamah watapokuwa Peponi. Yote haya ni haki. Mlango huu katika Qur-aan umezungumziwa sana. Kadhalika katika Hadiyth Swahiyh umezungumziwa sana. Mwenye kuizingatia Qur-aan na Sunnah basi atakuta hilo liko wazi katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuona kuwa vyote viwili vinamthibitishia sifa Allaah (´Azza wa Jall) ikiwa ni pamoja na ujuzi, uwezo, maneno, ujuu, radhi, ghadhabu, cheko na sifa za Allaah (Jalla wa ´Alaa) nyenginezo. Hivyo ni wajibu kumthibitishia nazo Allaah kwa njia inayolingana Naye (Subhaanahu wa Ta´ala). Inatakiwa kuzipitisha kama zilivyokuja pasi na kuzipotosha, kuzikanusha, kuziwekea namna na kuzilinganisha. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaona kuwa mlango huu ni mmoja na kwamba inatakiwa kuthibitisha ya kuwa ni haki na maana yake vilevile ni haki. Pamoja na hivyo hakuna anayejua namna zilivyo isipokuwa Yeye peke yake (Subhaanahu wa Ta´ala). Sambamba na hilo inatakiwa kutambua na kuamini kuwa hazifanani na sifa za viumbe:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

Kama ambavyo dhati ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) haifanani na dhati za viumbe, vilevile sifa Zake hazifanani na sifa za viumbe. Majina na sifa Zake zote ni haki. Ni wajibhu kumthibitishia navyo Allaah kwa njia inayolingana na Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hivi ndivyo alivyosema Maalik, Sufyaan ath-Thawriy, Ibn ´Uyaynah, Imaam Ahmad bin Hanbal, Ishaaq bin Raahuuyah, Imaam ash-Shaafi´iy na wengineo katika maimamu wa Uislamu. Mlango wao ni mmoja. Mlango ni mmoja: ni wajibu kuthibitisha Aayah na Hadiyth kuhusu sifa kama zilivyokuja kwa njia inayolingana na Allaah (Jalla wa ´Alaa) pasi na kupotosha, kukanusha, kuzifanyia mamna na kufananisha. Bali ni haki zimethibiti kwa Allaah (´Azza wa Jall). Sifa za Allaah hazifanani na sifa za viumbe Wake (Subhaanahu wa Ta´ala).

  • Mfasiri: Firqatunnajia.com