31. Ni ipi hukumu ya kupita mbele ya mwenye kuswali?

Swali 31: Ni ipi hukumu ya kupita mbele ya mwenye kuswali? Je, msikiti Mtakatifu wa Makkah unatofautiana na misikiti mingine katika jambo hilo? Nini maana kwamba mpitaji anakata swalah? Je, kwa mfano kunapopita mbele yake mbwa mweusi, mwanamke au punda aianze mwanzo?

Jibu: Hukumu ya kupita mbele ya mswaliji au kati yake yeye na Sutrah ni uharamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Laiti angelijua anayepita mbele ya mswaliji nini kinachompata basi ingelikuwa kusimama arobaini ni bora kwake kuliko kupita mbele ya anayeswali.”

Kuna maafikiano juu yake.

Ni jambo linalokata na kuiharibu swalah ikiwa mpitaji ni mwanamke ambaye ameshabaleghe, punda au mbwa mweusi. Ikiwa ambaye amepita ni vitu vingie mbali na hivi vitatu haviharibu swalah. Lakini kunapunguza thawabu zake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah ya mtu muislamu inakatika kusipokuwa mbele yake mfano wa bakora ya anayepanda kipando: mwanamke, punda na mbwa mweusi.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh).

Pia amesimulia Hadiyth mfano wake kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh). Lakini hakufungamanisha mbwa na weusi. Hadiyth iliyoachiwa inafasiriwa kwa Hadiyth iliyofungamanishwa kwa mujibu wa wanazuoni.

Msikiti Mtakatifu wa Makkah si haramu kupita mbele ya mwenye kuswali na wala hakikati swalah chochote katika vile vitu vitatu vilivyotajwa wala venginevyo. Kwa sababu ni maeneo pa msongamano na ni vigumu kuepuka kupita mbele ya mwenye kuswali. Kumepokelewa kuhusu hayo Hadiyth zinazosema waziwazi na ndani yake kuna unyonge. Lakini zinaungwa na yale mapokezi yaliyopokelewa juu ya hilo kutoka kwa Ibn-uz-Zubayr na wengineo. Jengine ni kwamba ni maeneo pa msongamano na kama tulivosema ni vigumu kuepuka kupita.

Msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mfano wake inapokuja katika maana na misikiti mingine kunapokuwa na msongamano mkubwa na ikawa ni vigumu kuejipusha na wapitaji. Amesema (´Azza wa Jall):

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Mcheni Allaah muwezavyo.”[1]

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

”Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”[2]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ninayokukatazeni basi jiepusheni nayo na nikikuamrisheni jambo basi lifanyeni muwezavyo.”

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

[1] 64:16

[2] 02:286

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 33-34
  • Imechapishwa: 23/08/2022