31. Mitihani inampelekea mtu kushukuru

Miongoni mwa manufaa yake ni kwamba inamfanya yule ambaye ameghafilika kutambua nafasi ya uzima. Kwa sababu mambo hayatambuliki isipokuwa kwa kutambua kinyume chake. Kwa hivyo kunapatikana kwa jambo hilo shukurani, kitu ambacho kitamzidishia neema. Kwa sababu mwishowe neema za Allaah, kukiwemo uzima, ni nyingi na kubwa kuliko mitihani na magonjwa Yake. Imepokelewa kwamba wakati wa Haatim al-Aswamm alikuwepo bwana mmoja akiitwa Mu´aadh mkubwa. Mu´aadh huyu mkubwa alipatwa na mtihani ambapo akakata tamaa, hivyo akaamrisha kuletwe wanawake wenye kuomboleza na kuvunjwa masahani. Wakati Haatim aliposikia jambo hilo, akaenda yeye pamoja na wanafunzi wake kumpa mkono wa pole. Akamwambia mmoja katika wanafunzi wake:

“ Wakati nitapokuwa nimeketi chini, basi niulize juu ya maana ya maneno Yake (Tabaarak wa Ta´ala):

إِنَّ الْإِنسَانَ لِرَبِّهِ لَكَنُودٌ

Hakika mtu kwa Mola wake bila shaka ni mkosefu mno wa shukurani.”[1]

Akamuuliza, ambapo akasema: “Hapa si mahali pa maswali.” Akamuuliza mara ya pili mara ya tatu, hatimaye akasema: “Hakika mtu ni mwenye kukufuru. Anahesabu misiba na anazisahau neema zake. Ni kama mfano wa Mu´aadh huyu! Allaah (Ta´ala) amemtunuku neema kwa miaka khamsini, lakini hakuna siku hata moja aliwakusanya watu ili kumshukuru Allaah (´Azza wa Jall) juu yake. Pindi alipofikwa na mtihani, akawakusanya watu kwa ajiliya kumlalamikia Allaah (Ta´ala).” Ndipo Mu´aadh akasema: “Ni kweli kabisa; hakika Mu´aadh ni mkosefu wa shukurani. Anayahesabu masaibu yake na anazisahau neema zake.” Baada ya hapo akaamrisha watoke wale wanawake wenye kuomboleza na akatubu juu ya kitendo chake hicho.”

[1] 100:6

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 114
  • Imechapishwa: 27/08/2023