31. Kitendo pekee ambacho kukiacha ni ukafiri

136 – al-Fadhwl bin Dukayn ametuhadithia: Hishaam bin Sa´d ametueleza, kutoka kwa Zayd bin Aslam[1], ambaye amesema:

”Watu wa dini hii ni lazima wafanye mambo manne: kuingia katika ulinganizi wa kiislamu, kuamini na kumsadikisha Allaah, Mitume, kuanzia wa mwanzo wao mpaka wa mwisho wao, Pepo na Moto na Kufufuliwa baada ya kifo, kufanya matendo yatayoisadikisha imani yako na kujifunza elimu itayoyafanya matendo yako kuwa mazuri.” Kisha akasoma:

وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِّمَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ

“Hakika Mimi ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia na akaamini na akatenda mema kisha akanyooka barabara.”[2]

137 – ´Abdul-A´laa ametuhadithia, kutoka kwa al-Jurayriy, kutoka kwa ´Abdullaah bin Shaqiyq[3], ambaye amesema:

”Hakuna kitendo ambacho mtu alikuwa anakiacha wanasema kuwa ni kufuru zaidi ya swalah. Walikuwa wakisema kuiacha swalah ni ukafiri.”

138 – Abu Bakr bin ´Ayyaash ametuhadithia, kutoka kwa Mughiyrah: Nilimuuliza bwana mmoja akimuuliza Shaqiyq[4]:

”Ulimsikia Ibn Mas´uud akisema yule mwenye kushuhudia kuwa ni muumini basi ashuhudie pia kuwa yuko Peponi?” Akasema: ”Ndio.”

139 – Abu Bakr bin ´Ayyaash ametuhadithia, kutoka kwa ´Aaswim, ambaye amesema:

”Kulisemwa kuambiwa Abu Waa-il: ”Wako watu wanadai kuwa waumini hawatoingia Motoni.” Akasema: ”Naapa kwa Allaah! Imejaa watu wasiokuwa waumini[5].”

140 – Abu Bakr amesema:

”Sisi tunaona kuwa imani ni maneno na vitendo. Inazidi na kushuka.”

Mwisho.

Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na amani zimwendee Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

[1] Ni Abu ´Abdillaah al-´Adawiy, mtumwa wa ´Umar aliyeachwa huru. Ni mwaminifu na mwanachuoni. Cheni ya wapokezi mpaka kwake ni Swahiyh.  

[2] 20:82

[3] Ni Abu ´Abdir-Rahmaan al-´Uqayliy. Alikuwa ni mwanafunzi wa Maswahabah na mwaminifu. Wasimuliaji wengine wa cheni ya wapokezi ni waaminifu na ni wanamme wa al-Bukhaariy na Muslim. Hata hivyo Sa´d bin Ayaas al-Jurayriy alikuwa akichanganya mambo miaka mitatu kabla ya kufa kwake. Kupitia kwake at-Tirmidhiy ameipokea na an-Nawawiy akasahihisha cheni ya wapokezi wake. al-Haakim ameipokea kupitia njia hiyohiyo isipokuwa tu yeye amezidisha kutoka kwa Abu Hurayrah. Ameisahihisha juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim na adh-Dhahabiy akasema kuwa cheni ya wapokezi wake ni njema. 

[4] Abu Waa-iyl al-Asdiy, mmoja katika wanafunzi wakubwa wa Maswababah. Cheni ya wapokezi kwenda mpaka kwake ni Swahiyh. Ameipokea Abu ´Ubayd katika “Kitaab-ul-Iymaan” (10-11).

[5] Bi maana Moto wa kudumu milele usiomalizika. Tazama (133).

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 49-50
  • Imechapishwa: 19/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy