30. Khatari ilioko kwa kuadhini kitambo kidogo kabla ya kuingia Fajr

Swali 30: Ni ipi hukumu ya kula na kunywa na huku muadhini anaadhini au baada ya adhaana kwa muda mchache na khaswa ikiwa mtu hajui kwa kulenga kuchomoza kwa alfajiri?

Jibu: Kipambanuo cha kukata kinachomzuia mfungaji kula na kunywa ni kule kuchomoza kwa alfajiri. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ ۚ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ

“Basi sasa changanyikeni nao [waingilieni] na tafuteni Aliyokuandikieni Allaah kwenu. Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni swawm mpaka usiku.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuleni na kunyweni mpaka aadhini Ibn Umm Maktuum. Kwani hakika yeye haadhini mpaka kuchomoze kwa alfajiri.”[2]

Kinachozingatiwa ni kuchomoza kwa alfajiri. Akiwa muadhini ni mwaminifu na anasema kuwa yeye haadhini mpaka kuingie alfajiri, basi mtu anatakiwa kujizuia pale tu anaposikia adhaana yake. Lakini ikiwa muadhini anaadhini kwa kujichunga, basi lililo salama zaidi kwa mtu ajizuie pale tu ataposikia adhaana ya muadhini. Isipokuwa kama yuko nchikavu na anaona alfajiri. Katika hali hiyo haimlazimu kujizuia ijapo anasikia adhaana mpaka aone alfajiri imechomoza ikiwa hakuna kizuizi kinachomzuia kuiona. Allaah amefungamanisha hukumu juu ya kubainika uzi mweupe kutokamana na uzi mweusi wa alfajiri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu adhaana ya Ibn Umm Maktuum:

“Kwani hakika yeye haadhini mpaka kuchomoze kwa alfajiri.”

Napenda kuzindua jambo linalofanywa na baadhi ya waadhini ambao wanaadhini dakika tano au dakika nne kabla ya kuingia kwa Fajr kwa madai ya kwamba eti kwa ajili ya usalama zaidi juu ya funga. Tunasema juu ya usalama huu kwamba ni ´kuchupa mpaka ` (تنطع) na si usalama uliowekwa na Shari´ah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wameangamia wenye kuchupa mpaka.”[3]

Ni usalama ambao si sahihi. Kwa sababu wakiweka usalama juu ya funga basi watazifanyia vibaya swalah. Watu wengi wanapomsikia muadhini basi wanasimama na kuswali Fajr. Katika hali hiyo huyu ambaye amesimama baada ya kusikia adhaana ya mwadhini ambaye ameadhini kabla ya swalah ya Fajr anakuwa ameswali swalah kabla ya wakati wake. Swalah kabla ya kuingia wakati wake si yenye kusihi. Jambo hilo ni kuwafanyia vibaya waswaliji.

Aidha ni kuwafanyia vibaya wafungaji. Kwa sababu anamzuia kula na kunywa yule ambaye anataka kufunga licha ya kuwa Allaah amemhalalishia jambo hilo. Kwa njia hiyo anakuwa amewafanyia tendo la jinai wafungaji kwa kuwazuilia jambo walilohalalishiwa na Allaah na waswaliji kwa vile wanakuwa wameswali kabla ya kuingia wakati wake, jambo ambalo linazibatilisha swalah zao.

Kwa hivyo ni lazima kwa waadhini wamche Allaah (´Azza wa Jall) na wafuate yale ya sawa katika kujichunga kwao kwa mujibu wa vile ilivyofahamisha Qur-aan na Sunnah.

[1] 02:187

[2] al-Bukhaariy (1918).

[3] Muslim (6878).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 48 mas-alatu fiy Swiyaam, uk. 29
  • Imechapishwa: 23/04/2021