29. Nia mpya kwa ajili ya kufunga kila siku ya Ramadhaan

Swali 29: Je, nia ya kufunga Ramadhaan inatosha mtu kutohitajia kuweka nia juu ya kila siku?

Jibu: Inafahamika kwamba kila mtu anasimama kuswali mwishoni mwa usiku na anakula daku. Hapana shaka kwamba amefanya hayo kwa sababu amekusudia kufunga. Kwa sababu kila mtu anafanya kitu kwa kutaka kwake mwenyewe. Hawezi kufanya isipokuwa kwa utashi. Utashi ndio nia yenyewe. Mtu hali mwishoni mwa usiku isipokuwa kwa sababu ya funga. Iwapo kula kwake ni kwa lengo la kula peke yake basi isingekuwa ni jambo la kimazowea kula katika wakati kama huu. Hii ndio nia.

Swali kama hili linahitajika pale ambapo kwa mfano tukadirie kama mtu amelala kabla ya kuzama kwa jua katika Ramadhaan na akaendelea kulala na asiamshwe na yeyote mpaka kukachomoza alfajiri katika siku ya pili, kwa msemo mwingine hakunuia sehemu ya usiku kufunga kwa ajili ya siku ya pili. Tuseme kuwa funga yake siku ya pili ni sahihi kujengea nia iliotangulia au tuseme kuwa funga yake si sahihi kwa sababu hakunuia sehemu ya usiku wake? Tunasema kuwa swawm yake ni sahihi. Maoni yenye nguvu ni kwamba inatosha kuweka nia pale mwanzoni mwa kufunga Ramadhaan na hakuna haja ya kufanya nia upya juu ya kila siku. Labda kama kutakuweko sababu inayomfanya mtu kufungua ambapo akafungua katikati ya mwezi. Katika hali hiyo ni lazima kuweka nia mpya kwa ajili ya kuanza tena kufunga.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 48 mas-alatu fiy Swiyaam, uk. 26-27
  • Imechapishwa: 23/04/2021