Miongoni mwa ´Aqiydah za Ahl-ul-Hadiyth ni kwamba imani ni maneno, matendo na utambuzi. Inazidi kwa utiifu na inapungua kwa maasi. Muhammad bin ´Aliy bin al-Hasan bin Shaqiyq amesema: ”Nilimuuliza Abu ´Abdillaah Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) maana ya imani kuzidi na kupungua. Akasema: ”al-Hasan bin Muusa al-Ashyab ametuhadithia: Hammaad bin Salamah ametuhadithia: Abu Ja´far al-Khatmiy ametuhadithia, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa ´Umayr bin Habiyb, aliyesema:

”Imani inazidi na kupungua.” Kukaulizwa kuhusu kuzidi na kupungua kwake ambapo akasema: ”Kuzidi kwake ni pale ambapo tutamtaja Allaah na kumuhimidi, na kupungua kwake ni pale ambapo tutaghafilika, kupuuza na kusahau.”

Abul-Hasan bin Abiy Ishaaq al-Muzakkaa ametukhabarisha: Baba yangu ametuhadithia: Abu ´Amr al-Hayriy ametuhadithia: Muhammad bin Yahyaa adh-Dhuhaliy, Muhammad bin Idriys al-Makkiy na Ahmad bin Shaddaad at-Tirmidhiy ametuhadithia: al-Humaydiy ametuhadithia: Yahyaa bin Sulaym ametuhadithia:

 ”Niliwauliza wanazuoni kumi kuhusu imani, ambapo wakajibu: ”Maneno na matendo.” Nikamuuliza Hishaam bin Hassaan, ambapo akajibu: ”Maneno na matendo.” Nikamuuliza Ibn Jurayj, ambapo akajibu: ”Maneno na matendo.” Nikamuuliza Sufyaan ath-Thawriy, ambapo akajibu: ”Maneno na matendo.” Nikamuuliza al-Muthannaa bin as-Swabbaah, ambapo akajibu: ”Maneno na matendo.” Nikamuuliza Muhammad bin ´Abdillaah bin ´Amr bin ´Uthmaan, ambapo akajibu: ”Maneno na matendo.” Nikamuuliza Muhammad bin Muslim at-Twaa-ifiy, ambapo akajibu: ”Maneno na matendo.” Nikamuuliza Fudhwayl bin ´Iyaadhw, ambapo akajibu: ”Maneno na matendo.” Nikamuuliza Naafiy bin ´Umar al-Jamhiy, ambapo akajibu: ”Maneno na matendo.”

Abu ´Amr al-Hayriy ametukhabarisha: Muhammad na Muhammad bin Idriys wametuhadithia: Nimemsikia al-Humaydiy akisema: Nimemsikia Sufyaan bin ´Uyaynah akisema:

”Imani ni maneno na vitendo, inazidi na kushuka.” Nduguye Ibraahiym bin ´Uyaynah akamwambia: ”Ee Abu Muhammad! Usiseme kuwa inashuka.” Akaghadhibika na kusema: ”Nyamaza, ee mtoto! Inashuka mpaka hakubaki chochote.”

al-Waliyd bin Muslim amesema:

”Nilimsikia al-Awzaa´iy, Maalik na Sa´iyd bin ´Abdil-´Aziyz wakimkaripia mwenye kusema ´Utambuzi bila matendo`. Wakasema: ”Hakuna imani pasi na matendo”

Ambaye utiifiu na matendo yake mema yatakuwa mengi, ndivo imani yake itakuwa kamilifu zaidi. Na ambaye utiifu wake utakuwa mchache, maasi na kupumbaa kwake kutakuwa kwingi, ndivo imani yake itazidi kuwa dhaifu.

Nimemsikia al-Haakim Abu ´Abdillaah al-Haafidhw akisema: Nimemsikia Abu Bakr Muhammad bin Ahmad bin Baakriyah al-Jallaad akisema: Nimemsikia Abu Bakr Muhammad bin Ishaaq bin Khuzaymah akisema: Nimemsikia Ahmad bin Sa´iyd ar-Ribaatiy akisema: ´Abdullaah bin Twaahir alinambia:

”Ee Ahmad! Hakika nyinyi mnawachukia watu hawa kwa ujinga na mimi nawachukia kwa utambuzi. Mosi ni kwamba hawaoni kufaa kumtii mtawala. Pili ni kwamba hawaithamini imani. Naapa kwa Allaah! Sijuzishi kusema kuwa imani yangu inalingana na imani ya Yahyaa bin Yahyaa wala imani ya Ahmad bin Hanbal, ilihali wao wanasema kuwa imani yao inalingana na imani ya Jabraaiyl na Mikaaiyl.”

Nimemsikia al-Haakim akisema: Nimemsikia Abu Ja´far Muhammad bin Swaalih bin Haani’ akisema: Nimemsikia Abu Bakr Muhammad bin Shu´ayb akisema: Nimemsikia Ishaaq bin Ibraahiym al-Handhwaliy akisema:

”Wakati Ibn-ul-Mubaarak alipofika Rayy, alisimama mfanya ´ibaadah mmoja, ambaye nadhani kuwa anafuata ´Aqiydah ya Khawaarij, akasema: ”Ee Abu ´Abdir-Rahmaan! Unasemae nini juu ya mtu ambaye anazini, anaiba na anakunywa pombe?” Akajibu: ”Simtoi nje ya imani.” Bwana yule akasema: ”Ee Abu ´Abdillaah! Umekuwa Murjiy na utuuzima wako?” Akajibu: ”Murj-ah hawanikubali. Murji-ah wanasema kuwa matendo yao mazuri yanakubaliwa na maovu yao ni yenye kusamehewa. Iwapo ningelijua kuwa mema yangu yamekubaliwa, basi ningejishuhudia kuwa niko Peponi.”

Kisha akasimulia kutoka kwa Abu Shawdhab, kutoka kwa Salamah bin Kuhayl, kutoka kwa Hudhayl bin Shurahbiyl, aliyesema kuwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Ingelipimwa imani ya Abu Bakr na imani ya wakazi wa ulimwengu, basi ingelikuwa na uzito zaidi.”

Nimemsikia Abu Bakr Muhammad bin ´Abdillaah bin Muhammad bin Zakariyyaa ash-Shaybaaniy akisema: Nimemsikia Yahyaa bin Mansuur al-Qaadhwiy akisema: Nimemsikia Muhammad bin Ishaaq bin Khuzaymah akisema: Nimemsikia al-Husayn bin Harb, nduguye Ahmad bin Harb az-Zaahid, akisema:

”Nashuhudia ya kwamba Ahmad bin Harb alikuwa akimwabudu Allaah kwa kuamini kuwa imani ni maneno na matendo na kwamba inazidi na kupungua.”

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 264-276
  • Imechapishwa: 18/12/2023