30. Anayopasa mfungaji kujiepusha nayo: Uwongo, upuuzi na ujinga

Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Ama baada ya hayo;

1 – Maneno ya upuuzi, ujinga na maneno ya uongo. Ni haramu kwa mwenye kufunga kuzungumza maneno ya upuuzi ambayo ni yale maneno machafu na vile vitangulizi vya jimaa, ugomvi, ujinga, maneno ya uongo na kuyatendea kazi na matusi. Akimtukana mtu au kupambana naye basi amweleze kuwa amefunga. Asimkabili kwa mfano wake. Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swawm ni ngao. Mmoja wenu akifunga asiseme maneno ya upuuzi na wala asigombane. Mtu akimtukana au kupambana naye, basi aseme: “Nimefunga.”[1]

Katika upokezi mwingine wa al-Bukhaariy kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swawm ni ngao. [Mfungaji] asiseme maneno ya upuuzi wala asifanye ujinga. Mtu akipambana naye au akamtusi, basi aseme: “Nimefunga.”[2]

Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyeeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule asiyeacha maneno ya uongo, kuyatendea kazi na ujinga, basi Allaah hana haja kwa yeye kuacha chakula na kinywaji chake.”[3]

[1] al-Bukhaariy (1904) na Muslim (1151).

[2] al-Bukhaariy (1894).

[3] al-Bukhaariy (1903).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Duruus fiy Ramadhwaan, uk. 48-49
  • Imechapishwa: 24/04/2023