Maneno kuhusu sura hii yamegawanyika sehemu mbili:

Ya kwanza: Umri ambao inakuja hedhi.

Ya pili: Muda wa hedhi.

1- Hedhi mara nyingi huja kuanzia miaka kumi na mbili mpaka miaka khamsini. Huenda mwanamke akapata hedhi kabla ya hapo au baada yake, kutegemea na hali yake, mazingira yake na hali yake ya hewa.

Wanachuoni wametofautiana kama kuna miaka maalum ambapo mwanamke anaweza kupata hedhi; anaweza kuipata kabla ya hapo au baada yake? Ile damu inayomtoka kabla ya miaka hiyo au baada yake inakuwa ni damu ya ugonjwa na sio damu ya hedhi? Kama tulivyosema wanachuoni wametofautiana katika hilo. ad-Daarimiy amesema baada ya kutaja tofauti zote hizo:

“Ninaona kuwa yote haya kwangu ni makosa. Yote yanazingatia katika kule kupatikana. Pasina kujali kiwango kitachopatikana, hali na miaka itawajibika kufanya hiyo kuwa ni hedhi na Allaah ndiye anajua zaidi.”[1]

Maoni haya ya ad-Daarimiy ndio ya sawa na vilevile ndio chaguo la Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah. Pale mwanamke atapoona hedhi yake basi atakuwa ni mwenye hedhi hata kama atakuwa ni chini ya miaka tisa au zaidi ya miaka khamsini. Kwa sababu Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamehusisha hukumu za hedhi kwa kule kupatikana kwake na sio kwa miaka maalum. Hivyo itakuwa ni wajibu kurejea katika kule kupatikana kwake ambapo zimehusishwa hukumu nayo. Kuiwekea hedhi miaka maalum ni kitu kinachohitajia dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah, jambo ambalo hakuna dalili ya hilo.

2- Wanachuoni wametofautiana tofauti kubwa juu ya muda wa hedhi katika kauli sita au saba. Ibn-ul-Mundhir amesema:

“Kuna wanachuoni waliosema kuwa hedhi haina kiwango cha uchache wake wala wingi wake kwa masiku maalum.”

Maoni haya ni kama maoni ya ad-Daarimiy. Hili pia ndio chaguo la Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah na ndio ya sawa kwa sababu inasapotiwa na Qur-aan, Sunnah na utafiti. Dalili ya kwanza ni Kauli ya Allaah (Ta´ala):

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ ۖ

“Na wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: “Hiyo ni dhara. Basi waepukeni wanawake [wanapokuwa] katika hedhi wala msiwakaribie [msijamiiane nao] mpaka watwaharike”.” (02:222)

Allaah akafanya kule kutwaharika ndio kikomo na hakufanya kikomo ni kwa idadi ya masiku maalum. Hili linatolea dalili kuonesha kuwa hukumu imehusishwa na kule kupatikana kwa damu ya hedhi na kukosekana; pale inapokuwepo, hukumu itathibiti, na inapokatika hukumu zake zinaondoka.

Dalili ya hili ni yale yaliyothibiti katika “as-Swahiyh” ya Muslim pale ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alipopata hedhi yake katika mnasaba wa ´Umrah:

“Fanya kila anachofanya mwenye kuhiji mbali na Twawaaf kwenye Ka´bah mpaka utwaharike.”

Akasema:

“Ilipofika ile siku ya kuchinja nikatwaharika.”[2]

al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia:

“Subiri. Utapotwaharika ndio wende Tan´iym.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akafanya kule kutwaharika ndio kikomo na si zama maalum. Hili linatolea dalili kuonesha kuwa hukumu imehusishwa na kule kupatikana kwa damu ya hedhi na kukosekana kwake.

Dalili ya tatu ni kwamba hivi viwango vya muda maalum vilivyotajwa na wanachuoni katika masuala haya hayapo katika Qur-aan na Sunnah pamoja na kuwa dharurah ni yenye kupelekea vikabainishwa. Lau ingelikuwa ni wajibu kwa waja kuyafahamu na kumuabudu Allaah kwavyo basi Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wangeliyabainisha kwa kila mtu. Kwa sababu hukumu muhimu ni zenye kupelekea katika hilo ikiwa ni pamoja na swalah, swawm, ndoa, talaka, mirathi na nyinginezo. Kwa mfano Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamebainisha idadi za swalah, nyakati zake, Rukuu na Sujuud, zakaah, mali zake, viwango vyake, kipimo chake, wanaostahiki kupewa, swawm na muda na zama zake, hajj na mengineyo ikiwa ni pamoja na adabu za kula, kunywa, kulala, jimaa, kukaa, kuingia nyumbani, kutoka nyumbani na adabu za kukidhi haja mpaka idadi ya kupangusa baada ya kujisaidia na yasiyokuwa hayo katika mambo ya ndani kabisa na ya wazi ambayo Allaah amekamilisha dini kwayo na akaitimiza neema Yake kwa waumini. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ

“Na Tumekuteremshia Kitabu kikiwa ni kielezo bayana cha kila kitu.” (16:89)

مَا كَانَ حَدِيثًا يُفْتَرَىٰ وَلَـٰكِن تَصْدِيقَ الَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَتَفْصِيلَ كُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ

“Haikuwa [Qur-aan] mazungumzo yanayozushwa – lakini ni ya kusadikisha [vitabu vilivyoitangulia] vya kabla yake na ufafanuzi wa kila kitu na ni mwongozo na Rahmah kwa watu wanaoamini.” (12:111)

Pindi viwango na ufafanuzi huu ulikuwa si wenye kubainishwa katika Qur-aan na Sunnah ikabainika kuwa ni mambo yasiyokuwa na mashiko na kwamba hedhi yenye kuhusishwa na hukumu za Kishari´ah badala yake inatakiwa kutundikwa na kule kupatikana kwake na kukosekana kwake. Dalili hii (bi maana kutokutajwa katika Qur-aan na Sunnah ni dalili ya kutokuzingatiwa kwake) itakunufaisha katika masuala haya na mambo mengine ya kielimu kwa sababu hukumu za Kishari´ah haziwi ni zenye kuthibiti isipokuwa kwa kupatikana dalili za Kishari´ah kutoka katika Qur-aan, Sunnah, maafikiano ya wanachuoni yenye kujulikana au kipimo sahihi. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Allaah amehusisha hukumu nyingi za hedhi katika Qur-aan na Sunnah na hakuweka kiwango cha wingi wake wala uchache wake wala kipindi cha kutwaharika kati ya hedhi mbili, pamoja na kuwa jambo hili ni lenye kugusa Ummah mzima na unalihitajia sana. Lugha haitofautishi kati ya kiwango fulani na kingine. Yule mwenye kuweka kikomo maalum ameenda kinyume na Qur-aan na Sunnah.”[4]

[1] al-Majmuu´ Sharh al-Muhadhdhab (1/386).

[2] Muslim (1211).

[3] al-Bukhaariy (1787).

[4] Majmuu´-ul-Fataawaa (19/35)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Dimaa’ at-Twabiy´iyyah lin-Nisaa’ http://www.ibnothaimeen.com/all/books/article_16961.shtml
  • Imechapishwa: 29/10/2016