6- Sahl bin al-Handhwaliyyah (Radhiya Allaahu ´anhu) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuomba na yeye yuko na cha kumtosheleza anajikusanyia Moto.” Kukasemwa: “Ee Mtume wa Allaah! Ni kipi cha kumtosheleza?” Akasema: “Chakula cha mchana na cha jioni.”[1]

7- Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anhu) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kuwaomba watu ilihali ana cha kumtosheleza atakuja siku ya Qiyaamah na uso wenye kuchubuka.” Kukasemwa: “Ee Mtume wa Allaah! Ni kipi chenye kutosheleza?” Akasema: “Sarafu khamsini ya fedha [dirhamu] au kiasi chake katika sarafu ya dhahabu [dinari].”[2]

Hadiyth nzuri zaidi katika mlango huu, kama alivosema ´Abdil-Barr, ni Hadiyth ya Sahl bin al-Handhwaliyyah.

8- Abu Bakr bin al-Athram ameeleza kuwa Ahmad bin Hanbal aliulizwa kuhusu kuomba na ni lini inajuzu. Akasema:

“Pale asipokuwa na chakula cha mchana wala cha jioni, kama ilivo katika Hadiyth ya Sahl bin al-Handhwaliyyah.” Akaulizwa ikiwa mtu amelazimika kuomba. Akajibu: “Inajuzu ikiwa amelazimika.” Akaulizwa ikiwa mtu ataacha kuomba katika hali hiyo. Akajibu: “Ni bora. Allaah Atamruzuku.” Kisha akasema: “Sidhani kama kuna mwenye kufa kwa sababu ya njaa.”

9- al-Athram amesema:

“Nilimsikia Ahmad akiulizwa juu ya mtu asiyepata chakula; ale nyamafu au aombe?” Akasema: “Je, ale nyamafu na wakati anaweza kuomba? Ni fedheha.”

[1] Ahmad (4/180), Abu Daawuud (1629) na Ibn Hibbaan (844).

[2] Ahmad (1/441), Abu Daawuud (1626), at-Tirmidhiy (645), an-Nasaa´iy (5/97) na Ibn Maajah (1840).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 16-18
  • Imechapishwa: 18/03/2017