3- Muslim amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuwaomba watu pesa ili awe na vingi hakika anaomba kaa la moto. Hivyo basi, mwache aombe vidogo au vingi.”[1]

Kuomba ili apate vingi ina maana ya kwamba anaomba pasina haja wala dharurah. Anaomba tu ili apate vingi. Hilo ni haramu. Haijuzu kuomba ikiwa ni pasina dharurah. Yule mwenye kuomba pasina haja anafanya kitendo ambacho ni haramu na anakula mali za watu kwa dhuluma kwa vile anadai ufakiri na kuchukua kitu ambacho si halali [kwake]. Kwa hivyo kunachelea juu yake akatumbukia Motoni.

Anaomba kaa la moto ina maana ya kwamba atakuja kulila kesho au kuunguzwa nalo. Mtu huyu anadai ufakiri ilihali Allaah (Ta´ala) Amemtajirisha. Badala ya kumshukuru Allaah kwa neema alizomneemesha anazikufuru. Anasema uongo pale anapoomba na anachukua swadaqah ambayo inawastahikia mafukara. Wao wana haki zaidi ya pesa hizi kuliko yeye. Wakati anapozichukua anakuwa amewapokosanya haki zao. Dhambi zote hizi chafu, zilizojificha na zenye kuonekana, zinapelekea katika adhabu Motoni. Yule mwenye kuchukua pesa kwa njia hii, zichukuliwe kutoka kwake na badala yake wapewe masikini na wengine. Asibakie nazo.

Mwache aombe vidogo au vingi ni matishio mengine ambayo ni makatazo na maonyo ya wazi. Haihusiani na kuwa na khiyari. Ni kama Kauli ya Allaah (Ta´ala):

فَمَن شَاءَ فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاءَ فَلْيَكْفُرْ

“Basi anayetaka aamini, na anayetaka akufuru.” (18:29)

4- Imepokelewa kwamba ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) alimsikia mwaombaji akisema:

“Mpeni chakula cha jioni mwombaji.” ´Umar akaamrisha apewe chakula. Kisha akageuka na kwenda kwenye nyumba ya ngamia na kusema: “Mpeni chakula cha jioni mwombaji.” ´Umar akasema: “Je, sikuwaambieni mumpe chakula cha jioni”? Wakasema: “Tulifanya hivo.” Akaamrisha aletwe. Akamwambia: “Je, hukupewa chakula?” Akasema: “Ndio.” ´Umar akachukua kifuko chake na kumwaga vyote mbele ya gamia za swadaqah na kusema: “Wewe sio mwombaji bali ni mkusanyaji.”

Wanachuoni wetu (Rahimahumu Allaah) wamesema:

Huoni jinsi ´Umar alivyoamrisha kupewa chakula kutokana na hali yake ya dhahiri? Alipoona kuwa anaomba ili aweze kupata vingi akaonelea kuwa sio mwenye kustahiki kupewa tena. Akachukua kile alichokusanya pasina haki na kukimwaga mbele ya ngamia za swadaqah. Fahamu hili ili – Allaah Akitaka – uweze kuelewa.

5- Abul-Aswad ad-Du´liy alimsikia mwombaji kwenye kilimo akisema:

“Allaah Amrehemu yule mwenye kumlisha mwenye njaa.” Akamwambia mtumwa wake: “Ni haki ya wajibu.” Akamwita, akakaa naye na kumlisha. Alipotoka akamsikia akisema hali kadhalika. Hivyo, akaamrisha arudishwe na kufungwa. Akamwambia: “Usiniombe kitu mpaka ifike asubuhi.”

[1] Muslim (1041), Ahmad (4637) na Ibn Maajah (1838).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 16-17
  • Imechapishwa: 18/03/2017