Pale ambapo watu wengi wamekuwa wenye kurudisha nyuma Sunnah kwa kutumia maoni yao binafsi na mapendekezo yao na miongoni mwa Sunnah zinazopingwa ni ile ya uwekwaji Shari´ah wa kuswali na viatu, ndipo nikaona nitaje baadhi ya dalili na maneno ya wanazuoni ambayo yanayobainisha ubaya wa njia hii na madhara yake katika dini. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwahukumu wanawake wawili wa kabila la Hudhayl waliogombana ambapo mmoja wao akampiga mwenzake jiwe, likampiga tumboni mwake akiwa mjamzito na kumuua mtoto aliyekuwa tumboni. Wakaleta mgogoro wao kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), naye akaamua kuwa fidia ya kilichokuwa tumboni ni mtumwa mwanaume au mjakazi. Walii wa mwanamke aliyelipa fidia akasema: “Vipi nilipie gharama ya yule ambaye hakunywa wala kula, hakuzungumza wala kulia kwa sauti? Hali kama hiyo inapaswa kupotea.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Hakika huyu ni miongoni mwa ndugu wa makuhani.”[1]

Kuna ziada imekuja kwa Muslim:

“Hakika huyu ni miongoni mwa ndugu wa makuhani kutokana na ushairi wake wa utungo.”[2]

al-Mughiyrah bin Shu´bah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Kuna mwanamke mmoja ambaye alimuua mwanamke mwenzake kwa kumpiga na mti wa hema. Wakampeleka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), naye akaamua fidia juu ya ndugu wa karibu wa muuaji na mwanamke huyo alikuwa mjamzito, hivyo akahukumu kutolewe mtumwa mwanaume au mjakazi juu ya kile kilichomo tumboni. Baadhi ya jamaa wa muuaji wakasema: “Tunalipa gharama ya yule ambaye hakula wala kunywa wala hakulia kwa sauti? Hali kama hiyo inapaswa kupotea.” Ndipo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): ”Huo ni ushairi kama ushairi wa mabedui?”[3]

Unaona namna Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyomkemea kwa ukali mtu aliyepingana na Hadiyth yake kwa kutumia maoni binafsi na akasema juu yake:

“Hakika huyu ni miongoni mwa ndugu wa makuhani kutokana na ushairi wake wa utungo.”

[1] al-Bukhaariy (5758) na Muslim (1681).

[2] Abu Daawuud (4/318), an-Nasaa’iy (8/43) na Ibn Maajah (2/882).

[3] Muslim (1681) na an-Nasaa’iy (8/44).

  • Muhusika: ´Allaamah Muqbil bin Haadiy al-Waadi´iy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: as-Swalaah fiyn-Ni´aal, uk. 33-34
  • Imechapishwa: 23/06/2025