29. Mitihani inakufanya uweze kuona ufalme wa Allaah

Mitihani ina faida kubwa na hekima za kiungu. Baadhi yake ziko wazi kwa kufikiria, baadhi ya neema zake zinatambulika. Nyenginezo hazionekani, lakini Allaah ameiwekea fadhilah nyingi. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

فَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَيَجْعَلَ اللَّـهُ فِيهِ خَيْرًا كَثِيرًا

“… pengine ikiwa mnachukia jambo na Allaah akalijaalia ndani yake kuwa na kheri nyingi.”[1]

Imaam Ahmad amepokea katika “az-Zuhd” kutoka katika Hadiyth za al-Hasan, ambazo kuna Swahabah anayekosekana katika cheni zake za wapokezi, ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Naapa kwa Allaah! Allaah hamuadhibu mpenzi Wake, lakini anaweza kumpa mtihani duniani.”[2]

Nasema:

Mtihani unapokuwa mzito zaidi unawepesishwa kwa kuridhika

na Allaah – mwema yuko na ridhaa

Ni neema ngapi zinazoambatana na mabalaa

watu hawazioni, lakini mitihani ni zawadi

Miongoni mwa faida za mitihani ni kutafakari ufalme wa Uola na kurejea katika kujisalimisha kwa ´ibaadah. Hakuna yeyote awezaye kuepuka amri na mipango ya Allaah. Wala hakuna yeyote awezaye kukimbia hukumu na mtihani Wake wenye kutekelezeka. Ni Wake Allaah ufalme na waja. Anafanya juu yetu kile anachokitaka na vile Anavyotaka. Hakika Kwake ndio marejeo yetu katika mambo yetu yote na Kwake ndio tutakusanyika atatukusanya kwa ajili ya kutufufua.

[1] 4:19

[2] az-Zuhd, uk. 71. Kuna Swahabah anayekosekana katika cheni ya wapokezi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 112-113
  • Imechapishwa: 23/08/2023