29. Majibu kwa njia nyingi kuonyesha kwamba mtu anaweza kukufuru hata kama ametimiza nguzo za Uislamu IX

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Yaweza kusemwa pia: “Wale ambao Allaah amesema juu yao:

يَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ مَا قَالُوا وَلَقَدْ قَالُوا كَلِمَةَ الْكُفْرِ وَكَفَرُوا بَعْدَ إِسْلَامِهِمْ

”Wanaapa kwa jina la Allaah kwamba hawakusema [maneno maovu]; ilihali wamesema neno la kufuru na wakakufuru baada ya Uislamu wao.” (at-Tawbah 09 : 74)

hamkusikia ya kwamba Allaah amewakufurisha kwa maneno yao, pamoja na kuwa walikuwa katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wakipigana Jihaad bega kwa bega pamoja naye, wakiswali pamoja naye, wakitoa zakaah pamoja naye, wakihiji na wakimpwekesha Allaah? Hali kadhalika wale ambao Allaah Kasema kuwahusu:

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema: Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?” Msitoe udhuru! Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.”” (at-Tawbah 09 : 65-66)

Watu hawa ambao Allaah kaweka wazi ya kwamba wamekufuru baada ya kuamini kwao – pamoja na kuwa wako na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika vita vya Tabuuk – walisema maneno ambayo walisema kuwa waliyasema kwa mzaha tu. Fikiria shubuha hii, nayo ni kauli yao: “Je, mnawakufurisha Waislamu ambao wanashuhudia hapana mungu isipokuwa Allaah, wanaswali na wanafunga”. Kisha fikiria jibu lake. Kwa hakika ni katika yamanufaa yaliyomo kwenye waraka hii.

Na katika dalili ya hayo pia ni yale Allaah (Ta´ala) aliyosema kuhusu Banuu Israaiyl –pamoja na Uislamu wao, elimu yao na wema wao – walimwambia Muusa: “Tufanyie mungu kama wao walivyo na waungu”. Hali kadhalika walisema baadhi ya Maswahabah: “Tujaalie Dhaat Anwaatw”. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaapa ya kwamba hii inakumbusha kauli ya Banuu Israaiyl: “Tufanyie mungu”.

Washirikina wana shubuha nyingine ambayo wanajaribu kuijadili kwa kisa hiki. Wanasema: “Kwa hakika Banuu Israaiyl hawakukufuru kwa hilo na hali hadhalika wale waliosema “Tufanyie Dhaat Anwaatw”, hawakukufuru”. Tunawajibu kwa kusema: “Banuu Israaiyl hawakufanya hilo, na hali kadhalika waliomuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawakufanya hilo. Na wala hakuna tofauti ya kwamba Banuu lau wangelifanya hilo wangelikufuru na wala hakuna tofauti ya kwamba wale aliowakataza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) lau wasingelimtii na wakachukua Dhaat Anwaatw baada ya makatazo, wangelikufuru. Na hili ndilo linalotakikana.

Lakini kisa hiki kinafidisha ya kwamba Muislamu wa kawaida, bali hata mwanachuoni, anaweza kutumbukia katika aina ya shirki bila ya kujua. Kinafidisha kujifunza na kuwa makini na kujua ya kwamba maneno ya mjinga “Tunajua Tawhiyd” ni katika ujinga mkubwa na hila za shaytwaan. Kinafidisha pia ya kwamba Muislamu mwenye kufanya Ijtihaad endapo atatamka neno la kufuru pasi na kujua. Akizinduliwa juu ya hilo na akutubia papo hapo, hakufuru, kama walivyofanya Banuu Israaiyl na wale waliomuomba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Na kinafidisha pia ya kwamba hata kama hakukufuru, anatakiwa kukemewa kwa makemeo makali kabisa, kama alivyofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

MAELEZO

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) anabainisha kwamba muislamu anapofanya kitu chenye kuwajibisha kuritadi anaritadi na kwamba maneno ya wajinga wanaosema kwamba sisi tunawakufurisha waislamu wenye kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, wanaswali na kwamba wanafunga, yote haya ni maneno ya kweli na ni ujinga mkubwa. Muislamu anapofanya kitu chenye kupelekea kwenye kuritadi anaritadi japokuwa anaswali na anafunga. Amesema (´Azza wa Jall):

يَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ مَا قَالُوا وَلَقَدْ قَالُوا كَلِمَةَ الْكُفْرِ

“Wanaapa kwa Jina la Allaah kwamba hawakusema na hali wamekwishasema neno la kufuru.”[1]

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?”  Msitoe udhuru; mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.”[2]

Walikuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini pamoja na hivo walitamka maneno ya kufuru na wakakufuru baada ya Uislamu wao. Mtu akifanya jambo la ukafiri, hata kama atakuwa ni miongoni mwa watu wenye kuabudu zaidi, anakufuru na anatoka nje ya Uislamu na kwenda katika mzunguko wa ukafiri. Kwa ajili hii maimamu wote wametunga mlango kwa jina “Hukumu ya mwenye kuritadi” ambaye ni muislamu aliyeritadi baada ya Uislamu wake. Kadhalika wana wa israaiyl walisema:

اجْعَل لَّنَا إِلَهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ

“Tufanyie mungu kama ambavyo wao wako na miungu!”[3]

Vilevile baadhi ya waislamu walipokuwa njiani wanaelekea Hunayn walisema:

“Tujaalie Dhaat Anwaatw kama wao walivyo na Dhaat Anwaatw.”

Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Allaah ametakasika kutokamana na mapungufu! Hivi ndivo walivyosema watu wa Muusa:

اجْعَل لَّنَا إِلَهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ

“Tufanyie mungu kama ambavyo wao wako na miungu!”

“Ninaapa kwa Yule ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake. Hakika mtafuata mienendo ya wale waliokuwa kabla yenu.”[4]

Walifikiria kuwa jambo hili linafaa na halina neno. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawazindua kwamba ni kosa kubwa. Iwapo wangelikwenda kinyume na wakafanya Dhaat Anwaatw wangelikufuru. Kadhalika wana wa israaiyl lau wangelimwabudu mungu na wasinasihike wangelikufuru.

Kwa kifupi ni kwamba visa hivi ndani yake kuna ubainifu na hoja ya wazi juu ya ukafiri wa mwenye kufanya jambo la ukafiri. Lakini yule mwenye kufanya kitu akidhani kuwa ni haki kisha akazinduka hakufuru kwa ujinga wake. Ikiwa muislamu anajahili kitu kama hicho basi ni juu yake kutubu na kurejea kwa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Mwenye kutubu basi Allaah anamsamehe. Mtu anaweza kutumbukia kwenye ukafiri kutokana na sababu nyingi. Miongoni mwa sababu hizo ni ujinga, matamanio, tamaa za mambo ya kidunia au kumtii ambaye anaona inafaa kumtii. Akizinduliwa na akatubu kwa Allaah basi tawbah inasihi japokuwa itakuwa ni miongoni mwa madhambi makubwa kabisa. Kila dhambi ina tawbah yake. Dhambi kubwa kabisa ni shirki. Mwenye kutubia Allaah anamsamehe. Wapo kundi kubwa la wakuu wa makafiri wa Quraysh waliokuwa juu ya ukafiri kisha Allaah akawaongoza na wakawa miongoni mwa watu bora kabisa baada ya kusilimu na kuongozwa na Allaah (´Azza wa Jall). Miongoni mwao wako ambao walisilimu baada ya Hudaybiyah, wako ambao wamesilimu baada ya kukombolewa mji wa Makkah. Walifanya hivo baada ya ukafiri mkubwa na kuwapiga vita Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah. Baadhi yao ni Abu Sufyaan ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa makafiri siku ya Uhud na Khandak. Pamoja na haya akaingia katika Uislamu na akawa (Radhiya Allaahu ´anh) ni miongoni mwa watu bora baada ya hapo. Mwengine ni ´Ikrimah bin Abiy Jahl, Swafwaan bin Umayyah na wengineo.

[1] 09:74

[2] 09:65-66

[3] 07:138

[4] at-Tirmidhiy (2180) na Ahmad (21947).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 101-103
  • Imechapishwa: 25/10/2021