29. Kula kwa wingi kunaidhoofisha miili

151 – ´Awn bin Ibraahiym amenihadithia: Ahmad bin Abiyl-Hawaariy amenihadithia: ´Abdullaah bin as-Sariy amenihadithia:

”Kuna kijana mmoja alikuwa anafanya ´ibaadah huko Baswrah na shangazi yake alikuwa akimtumia chakula. Kwa muda wa siku tatu hakumwagizia chochote, ambapo akasema: ”Ee Mola, umeniondoshea riziki yangu?” Tahamaki akarushiwa mfuko wa uji kwenye kona ya msikiti, na akaambiwa: ”Hebu hii hapa, ee mchache wa subira!” Ndipo akasema: ”Naapa kwa utukufu Wako! Kwa vile Umenikaripia, basi sintokionja.”

152 – Abu Bakr bin Ismaa´iyl at-Taymiy amenihadithia: ar-Rabiy´ bin Naafiy´ ametuhadithia: ´Atwaa’ bin Muslim ametuhadithia:

”Yalipotea matumizi ya Ibraahiym bin Ad-ham, ambapo akawa anakula changarawe kwa muda wa siku kumi na tano.”

153 – al-Qaasim bin Zakariyyaa bin Diynaar al-Qurashiy ametuhadithia: Abu Yaziyd al-Mu´laa ametuhadithia: Twu´umah bin ´Amr ametuhadithia:

”Ibraahiym bin Ad-ham alikuja akiwa na njaa, ambapo akala udongo matonge matatu.”

154 – Yahyaa bin Twalhah al-Yarbuu´iy ametuhadithia: Fudhwayl bin ´Iyaadhw ametuhadithia, kutoka kwa Maalik bin Diynaar, ambaye amesema:

”Nilisema kumwambia Muhammad bin Waasiy´: ”Pepo kwa ambaye yuko na kipato cha chini.” Ndipo Muhammad akasema: ”Pepo kwa ambaye ameamka akiwa na njaa na Allaah yuko radhi naye.”

155 – Muhammad bin al-Husayn amenihadithia: Khalaf bin Ismaa´iyl amenihadithia:

”Bwana mmoja katika watu wenye hekima kutoka India alinambia: ”Kula sana kunaudhoofisha mwili.”

156 – Muhammad amenihadithia: Ahmad bin Sahl al-Urduniy amenihadithia: Nimemsikia ´Abbaad bin ´Abbaad ar-Ramliy akisema:

”Ilikuwa inasemwa kwamba kula sana kunapoteza ufahamu na kunapelekea ususuwavu na usingizi.”

157 – Muhammad amesema: Muhammad bin Ja´far al-Madaa-iniy ametuhadithia, kutoka kwa Bakr bin Khunays, kutoka kwa Abu ´Abdillaah ash-Shaamiy, kutoka kwa Mak-huul, ambaye amesema:

”´Ibaadah bora baada ya zile za faradhi, njaa na kiu.”

Bakr bin Khunays amesema:

”Ilikuwa inasemwa kwamba njaa na kiu kunamfanya mtu kufahamu vyema zaidi mawaidha na kunaulainisha moyo upesi zaidi. Ilikuwa pia inasemwa kwamba kula sana kunazuia kheri nyingi.” 

158 – Ziyaad bin Ayyuub ametuhadithia: Ahmad bin Abiyl-Hawaariy ametuhadithia: Nimemsikia Abu Sulaymaan ad-Daaraaniy akisema: Nimemsikia Abul-Ash-hab, swahiba yake al-Hasan huko ´Abbaadaan, akisema:

”Allaah (´Azza wa Jall) alimfunulia wahy Daawuud (´alayhis-SalaamI): ”Ee Daawuud! Jihadhari na waonye maswahabah wako kutokana na matamanio ya chakula. Kwani hakika mioyo iliyofungamana na matamanio ya kidunia, ni yenye kuzuiwa kutokana Nami.”

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Juu´, uk. 100-103
  • Imechapishwa: 25/07/2023