29. Imani ya kati na kati na imani iliyokamilika

127 – Abu Mu´aawiyah ametukhabarisha, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Abu Swaalih, kutoka kwa ´Abdullaah bin Dhamrah, kutoka kwa Ka´b, ambaye amesema:

”Mwenye kusimamisha swalah na kutoa zakaah, basi amekuwa na imani ya kati na kati.”[1]

128 – Muhammad bin ´Ubaydillaah ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Abu Swaalih, kutoka kwa ´Abdullaah bin Dhamrah, kutoka kwa Ka´b, ambaye amesema:

”Mwenye kusimamisha swalah, akatoa zakaah na akamtii Muhammad, basi amekuwa na imani ya kati na kati. Yule mwenye kupenda kwa ajili ya Allaah, akachukia kwa ajili ya Allaah na akazuia kwa ajili ya Allaah, basi ameikamilisha imani.”[2]

129 – Ismaa´iyl bin ´Ayyaas ametuhadithia, kutoka kwa ´Ubaydullaah bin ´Ubaydillaah al-Kulaa´iy[3], ambaye amesimulia:

”Mak-huul alinishika mkono na kusema: ”Ee Abu Wahb, unasemaje juu ya mtu ambaye ameacha swalah ya faradhi kwa makusudi?” Nikasema: ”Ni muumini aliyeasi.” Akanifinya kwenye mkono wangu na kusema: ”Ee Abu Wahb, itukuze imani kwenye moyo wako! Yule mwenye kuacha swalah ya faradhi kwa makusudi, basi amekosa ulinzi wa Allaah. Na yule mwenye kukosa ulinzi wa Allaah basi amekufuru.”

130 – Abu Khaalid al-Ahmar ametuhadithia, kutoka kwa ´Amr bin Qays[4], kutoka kwa Abu Ishaaq, kutoka kwa ´Aliy (Rahimahu Allaah), ambaye amesema:

”Mafungamano ya subira kwa imani ni kama mafungamano ya kichwa kwa kiwiliwili. Ikiondoka subira basi inaondoka imani.”

[1] Cheni ya wapokezi ni nzuri. Wapokezi ni waaminifu na ni wanamme wa al-Bukhaariy na Muslim isipokuwa tu Ibn Dhamrah, ambaye al-´Ijliy amemuona kuwa ni mwaminifu na Ibn Hibbaan na isitoshe kuna jopo la waaminifu wamepokea kutoka kwake. Maneno yake ”Yule mwenye kupenda kwa ajili ya Allaah… ” imesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ameipokea Abu Daawuud na at-Tirmidhiy. Nimeihakiki katika “as-Swahiyhah” (375).

[2] Cheni ya wapokezi ni nzuri.

[3] Imekuja katika ile ya asili ”´Abdullaah”. Masahihisho yamefanywa kutokana na ”al-Muswannaf” na vitabu vya nyasifu. Cheni ya wapokezi ni Swahiyh. Baadhi ya matamshi yamepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kupitia kwa Sa´iyd bin ´Abdil-´Aziyz, kutoka kwa Mak-huul, kutoka kwa Umm Ayman, ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Usiache swalah kwa makusudi. Kwani mwenye kuacha swalah kwa makusudi, basi amekosa ulinzi wa Allaah na Mtume Wake.” (Ahmad (6/421))

Wapokezi wake ni waaminifu isipokuwa Mak-huul hakumsikia Umm Ayman, hivo ndivo alivosema al-Mundhiriy katika “at-Targhiyb wat-Tarhiyb” (1/197). Mfano wake imekwishatangulia kutajwa kutoka kwa Jaabir (44) na Buraydah bin al-Haswiyb (46).

[4] Ni Malaa´iy al-Kuufiy. Alikuwa ni mwaminifu. Vivyo hivyo kuhusu wapokezi wengine isipokuwa Abu Ishaaq as-Sabi´iy, ambaye alichanganyikiwa, hakuwahi kumsikia ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) na isitoshe alikuwa ni mudallis.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 47-48
  • Imechapishwa: 18/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy