28. Kutawadha ni nusu ya imani

122 – Wakiy´ ametuhadithia: al-Awzaa´iy ametueleza, kutoka kwa Hassaan, kutoka kwa ´Ikrimah, ambaye amesema:

”Wudhuu´ ni nusu ya imani.”

123 – Wakiy´ ametukhabarisha: Sufyaan ametueleza, kutoka kwa Abu Ishaaq, kutoka kwa Ibn Abiy Laylaa al-Kindiy[1], kutoka kwa mmoja katika wana wa Hujr, aliyeeleza:

”Hujr alimuona mmoja katika wana wake akitoka msalani akasema: ”Ee kijana! Nipe jani. Nilimsikia ´Aliy akisema: ”Usafi ni nusu ya imani.”

124 – Muhammad bin Bishr ametuhadithia: Zakariyyaa al-Hawaariy[2] ametueleza kwamba ´Abdullaah bin ´Amr amesema:

”Mzizi wa dini na nguzo zake ni swalah, zakaah – haviachani – kuhiji Nyumba na kufunga Ramadhaan. Miongoni mwa matendo bora kabisa ni swadaqah na jihaad.”

Kisha akasimama na kuondoka zake.

125 – Ibn ´Ulayyah ametukhabarisha, kutoka kwa Yuunus, kutoka kwa al-Hasan, ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Muumini mwenye imani kamilifu zaidi ni yule mwenye tabia njema zaidi katika wao.”[3]

126 – Ibn Numayr ametuhadithia: Muhammad bin Abiy Ismaa´iyl ametueleza, kutoka kwa Ma´qal al-Khath´amiy, ambaye amesema:

”Bwana mmoja alimjia ´Aliy akiwa Rahbah akasema: ”Ee kiongozi wa waumini! Unasemaje juu ya mwanamke asiyeswali?” Akasema: ”Asiyeswali ni kafiri.”[4]

[1] Imekuja namna hii katika ile ya asili na katika ”al-Muswannaf”, tofauti na ile sehemu iliyotangulia. Simjui katika wapokezi ambaye anaitwa Ibn Abiy Laylaa al-Kindiy. ´Abdur-Rahmaan bin Abiy Laylaa al-Answaariy al-Kuufiy ni mwaminifu, lakini hatokei Kind. Ibn Abiy Haatim hakumtaja mwingine aliyesimulia kutoka kwa Hudjr bin ´Adiy isipokuwa tu huyu Abu Laylaa al-Kindiy. Allaah ndiye anayejua zaidi. Lakini imekuja katika ”at-Tahdhiyb” ya kwamba kuna wengi, akiwemo huyu Abu Ishaaq, ambaye ndiye as-Sabiy´iy, wamepokea kutoka kwake. Hili ni miongoni mwa mambo yanayotilia nguvu masahihisho yangu ya punde tu, ya kwamba bwana huyo alikuwa Abu Laylaa al-Kindiy.

[2] Simjui. as-Sam´aaniy hakumtaja yeyote kwa nisba hii ambaye yuko katika tabaka hili. 

[3] Swahiyh. Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh na inayokosa Swahabah. Imekwishatangulia kutajwa hali ya kuwa na cheni iliyoungana kupitia kwa Abu Hurayrah na ´Aaishah (17-20).

[4] Hayakusihi kutoka kwa ´Aliy wa sababu ya huyu Ma´qal. Alikuwa hatambuliki kwa mtazamo wa Haafidhw Ibn Hajar katika ”at-Taqriyb”.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 46
  • Imechapishwa: 18/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy