72 – Qutaybah bin Sa´iyd ametuhadithia: al-Layth ametuhadithia, kutoka kwa Abuz-Zubayr, kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh), ambaye amesema:

”Bwana anayetokana na Banuu ´Udhrah aliachia huru mtumwa wake ambaye alikuwa akijaribu kununua uhuru wake. Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofikiwa na khabari hiyo, akasema: ”Je, unayo mali nyingine zaidi ya hiyo?” Akasema: ”Hapana.” Ndipo Mtume wa Allaah akasema: ”Ni nani atayemnunua kutoka kwangu?” Nu´aym bin ´Abdillaah an-Nahhaam akamnunua kwa dinari 800. Akaja nazo kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumlipa. Kisha akasema: ”Anza na nafsi yako na ujitolee swadaqah.” Kukibaki kitu kutoka kwa jamaa zako, basi umpe fulani na fulani. Bi maana mbele yako, kuliani mwako na kushotoni mwako.”

73 – Aadam bin Abiy Iyaas ametuhadithia: Shu´bah ametuhadithia: Ibn Abiy Dhi’b amesema: Sa´iyd bin Sam´aan ametuhadithia:

”Nimemsikia Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) akiomba kinga dhidi ya uongozi wa vijana na watenda madhambi.” Sa´iyd bin Sam´aan akasema: ”Ibn Hasanah al-Juhaniy akanikhabarisha kwamba alimwambia Abu Hurayrah: ”Ni ipi alama ya hilo?” Akasema: ”Kizazi kukatwa, wapotofu kutiiwa na wenye kuongoza wakaasiwa.”

74 – Muhammad bin ´Abdil-Waahid bin ´Uyaynah bin ´Abdil-Waahid ametuhadithia: Babu yangu amenihadithia, kutoka kwa Bayaan bin Bishr, kutoka kwa Qays bin Abiy Haazim, kutoka kwa ´Amr bin al-´Aasw (Radhiya Allaahu ´anh), ambaye amesema:

”Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiita kwa sauti ya juu na sio ya kimyakimya: ”Hakika hapana vyenginevyo walii wangu ni wale walioamini, lakini wako na jamaa ambao nitawaunga na kuwaangalia.”

75 – Aadam bin Abiy Iyaas ametuhadithia: Shu´bah ametuhadithia, kutoka kwa Sulaymaan at-Taymiy: Nimemsikia Abu ´Uthmaan an-Nahdiy, kutoka kwa Usaamah bin Zayd, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye amesema:

”Sijaacha nyuma yangu fitina yenye madhara zaidi kwa wanaume kama wanawake.”[1]

**

Mwisho. Himdi zote njema ni stahiki ya Allaah kwa hali zote.

Kimeandikwa kwa ajili ya matumizi ya kibinafsi na mtumwa Muhammad Mansuur bin ´Aliy al-Husayniy al-Halabiy, jumanne 28 Shawwaal 887 Azhar, Cairo – Allaah ailinde.

Ee Allaah! Msifu na msalimu bwana wetu Muhammad, jamaa zake na Maswahabah zake.

[1] al-Bukhaariy (4808) na Muslim (2741).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Ismaa´iyl al-Bukhaariy (a.f.k 256)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Birr-ul-Waalidayn, uk. 164-167
  • Imechapishwa: 21/01/2025