Isitoshe al-Jahm anadai kitu kingine; anauliza kama Qur-aan ni kitu. Tukisema kuwa ni kitu, anasema:

”Allaah ameumba kila kitu. Ni kwa nini basi Qur-aan isiwe miongoni mwa vile vitu vilivyoumbwa? Kwani nyinyi mmekiri wenyewe kuwa Qur-aan ni kitu.”

Alimakinika kwa madai hayo na hivyo akawatia watu mchanga wa machoni. Hata hivyo Allaah ndani ya Qur-aan hakuyaita maneno yake kuwa ni kitu, isipokuwa tu yale yanayokuwa kwa maneno Yake. Hukumsikia Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) akisema:

إِنَّمَا قَوْلُنَا لِشَيْءٍ إِذَا أَرَدْنَاهُ أَن نَّقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

“Hakika si vyenginevyo kauli Yetu juu ya kitu tunapokitaka hukiambia: “Kuwa!” – basi kinakuwa.”[1]

Kitu sio yale maneno Yake, isipokuwa kitu ni kile kilichokuwa kwa maneno Yake. Amesema (Ta´ala) katika Aayah nyingine:

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

”Hakika si vyenginevyo amri Yake anapotaka jambo lolote huliambia: “Kuwa!” nalo huwa.”[2]

Kitu sio ile amri Yake, isipokuwa kile kitu kilichokuwa kutokana na amri Yake.

Aidha inatambulika kuwa hakukusudia kuyaingiza maneno Yake ndani ya vile vitu vilivyoumbwa. Kwa mfano Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu ule upepo ambao aliutuma dhidi ya kina ´Aad:

تُدَمِّرُ كُلَّ شَيْءٍ بِأَمْرِ رَبِّهَا فَأَصْبَحُوا لَا يُرَىٰ إِلَّا مَسَاكِنُهُمْ

“Unaangamiza kila kitu kwa amri ya Mola wake. Wakapambaukiwa hayaonekani isipokuwa majengo yao.”[3]

Hata hivyo upepo ule haukukiharibu kila kitu. Nyumba na makazi yao vilibaki. Vivyo hivyo milima iliokuwa pambizoni mwake, licha ya kwamba Amesema:

تُدَمِّرُ كُلَّ شَيْءٍ بِأَمْرِ رَبِّهَا

“Unaangamiza kila kitu kwa amri ya Mola wake.”

Mambo ni vivyo hivyo pale anaposema (Ta´ala):

لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ

”Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye Muumbaji wa kila kitu.”[4]

Hakusudii Yeye Mwenyewe, ujuzi Wake wala maneno Yake anapotaja vitu vilivyoumbwa. Amesema kuhusu malkia wa Saba´:

وَأُوتِيَتْ مِن كُلِّ شَيْءٍ

”… na amepewa kila kitu… ”[5]

Lakini miongoni mwa vitu ambavo alikuwa hakupewa ni ufalme wa Sulaymaan (´alayhis-Salaam). Vivyo hivyo anaposema:

لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ

”Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye Muumbaji wa kila kitu.”

hakusudii kuyaingiza maneno Yake ndani ya vile vitu vilivyoumbwa.

Allaah (Ta´ala) amesema kumwambia Muusa (´alayhis-Salaam):

وَاصْطَنَعْتُكَ لِنَفْسِي

“Nimekuchagua kwa ajili Yangu.”[6]

وَيُحَذِّرُكُمُ اللَّـهُ نَفْسَهُ

“Allaah anakutahadharisheni na nafsi Yake.”[7]

كَتَبَ رَبُّكُمْ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ

”Mola wenu amekidhia juu ya Nafsi Yake rehema.”[8]

تَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِي وَلَا أَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِكَ

”Unayajua yale yote yaliyomo katika nafsi yangu na wala [mimi] sijui yale yaliyomo katika Nafsi Yako.”[9]

Amesema tena (Ta´ala):

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ

”Kila nafsi itaonja mauti.”[10]

Licha ya kwamba Yeye (´Azza wa Jall) amesema kuwa kila nafsi itaonja mauti, anapata kufahamu kila mtu mwenye akili kwamba hakusudii kuijumuisha nafsi Yake pamoja na nafsi hizo. Vivyo hivyo anaposema:

لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ

”Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye Muumbaji wa kila kitu.”

Hamaanishi Yeye Mwenyewe, ujuzi Wake wala maneno Yake pamoja na hivyo vitu vilivyoumbwa.

Hapa kuna dalili na ubainifu kwa yule ambaye Allaah amemtunuku akili. Allaah amrehemu ambaye anafikiri, anajirejea kutokana na maoni yake yanayoenda kinyume na Qur-aan na Sunnah na asiseme kuhusu Allaah isipokuwa kilicho haki. Allaah alichukua ahadi kutoka kwa viumbe Wake pale aliposema:

أَلَمْ يُؤْخَذْ عَلَيْهِم مِّيثَاقُ الْكِتَابِ أَن لَّا يَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ إِلَّا الْحَقَّ

”Je, halikuchukuliwa kwao fungamano la Kitabu kwamba wasiseme kumuhusu Allaah isipokuwa haki?[11]

Akasema katika Aayah nyingine:

قُلْ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ وَالْإِثْمَ وَالْبَغْيَ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَأَن تُشْرِكُوا بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ

“Sema: “Hakika si vyenginevyo Mola wangu ameharamisha machafu, yaliyodhihirika na yaliyofichika na dhambi [aina zote] na ukandamizaji bila ya haki na [ameharamisha] kumshirikisha Allaah kwa ambayo hakukiteremshia mamlaka na kuzungumza juu ya Allaah yale ambayo hamyajui.”[12]

Allaah ameharamisha kuzungumzwa uwongo juu yake. Amesema:

وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ تَرَى الَّذِينَ كَذَبُوا عَلَى اللَّـهِ وُجُوهُهُم مُّسْوَدَّةٌ ۚ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْمُتَكَبِّرِينَ

”Na siku ya Qiyaamah utawaona wale waliomsingizia uwongo Allaah nyuso zao zimepiga weusi. Je, kwani si katika Jahannam ndio makazi kwa ajili ya wanaofanya kiburi?”[13]

Allaah atulinde sisi na nyie kutokana na fitina zinazopotosha[14]!

[1] 16:40

[2] 36:82

[3] 46:25

[4] 6:102

[5] 27:23

[6] 20:41

[7] 3:28

[8] 6:54

[9] 5:116

[10] 3:185

[11] 7:169

[12] 7:33

[13] 39:60

[14] Ibn ´Aqiyl al-Hanbaliy amesema:

”Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ameandika kitabu kinachoitwa ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah wal-Qadariyyah.” (al-Aadaab ash-Shar´iyyah (1/274))

Ibn Taymiyyah amesema:

”Kama alivosema Imaam Ahmad katika kitabu chake ”ar-Radd ´alaaz-Zanaadiqah wal-Jahmiyyah.”  (Tafsiyr Suurat-il-Ikhlaasw, uk. 239)

Ibn Kathiyr amesema:

”… na hivo ndivo alivosema Ahmad bin Hanbal katika kitabu ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah” (Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (3/304))

Ibn Hajar al-´Asqalaaniy amesema:

”Amesema waziwazi Ahmad katika kitabu “ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah.” (Fath-ul-Baariy (13/598))

  • Mhusika: Imaam Ahmad bin Hanbal (afk. 241)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 113-117
  • Imechapishwa: 22/04/2024