28. Sifa muhimu na kuu zaidi kwa mlinganizi

Miongoni mwa tabia muhimu zaidi na kubwa zaidi kwa mlinganizi ni yeye atendee kazi yale anayoyalingania na akomeke na yale anayoyakataza na awe mwenye maadili mema, wasifu mzuri, mwenye subira, kujisubirisha, kumtakasia nia Allaah katika ulinganizi wake, kujitahidi katika ile kheri anayowafikishia watu na katika ile batili anayowaweka nayo watu mbali. Licha ya haya yote awaombee uongofu. Hii ni moja ya tabia njema awaombee uongofu na amwambie yule anayemlingania:

“Allaah akuongoze, akuwafikishe kuikubali haki na akusaidie kuikubali haki.”

Mwombee du´aa, mwelekeze na uwe na subira juu ya maudhiko. Licha ya hayo umwombee uongofu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema wakati alipoambiwa kuwa Daws wameasi ambapo akasema:

“Ee Allaah! Waongoze Daws na uwalete.”[1]

Mwombee uongofu na kuwafikishwa kuikubali haki. Unatakiwa vilevile ufanye subira na ujisubirishe juu ya hayo. Usikate tamaa na usivunjike moyo na wala usiseme isipokuwa kheri tupu. Usifanye jeuri na wala usiseme maneno mabaya yanayowakimbiza watu kutokana na haki. Lakini ambaye anadhulumu na kuchupa mpaka jambo lake ni jingine. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَلَا تُجَادِلُوا أَهْلَ الْكِتَابِ إِلَّا بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ إِلَّا الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْهُمْ

“Na wala msijadiliane na Ahl-ul-Kitaab isipokuwa kwa yale ambayo ni mazuri zaidi; isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao.”[2]

Dhalimu ambaye anakabili ulinganizi kwa shari, ukaidi na maudhiko hukumu yake ni nyingine. Kama inawezekana atiwe adabu kwa hilo kwa kufungwa au kitu kingine na kutiwa kwake adabu kuwe kwa kutegemea zile ngazi za dhuluma. Lakini muda wa kuwa ni mwenye kujizuilia maudhiko basi ni lazima kwako kumsubiria, utarajie malipo na ujadiliane naye kwa njia iliyo bora zaidi, puuzilia mbali yale yanayohusiana na utu wako kunako baadhi ya maudhiko. Hivo ndivo walivosubiri Mitume na wale waliowafuata kwa wema.

Swalah, amani na baraka zimwendee mja na Mtume Wake; Mtume wetu Muhammad, kizazi chake, Maswahabah zake na wale waliowafuata kwa wema mpaka siku ya Malipo.

[1] al-Bukhaariy (937) na Muslim (2524).

[2] 29:46

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 47-48
  • Imechapishwa: 14/06/2023