27. Mlinganizi asiyetendea kazi yale anayoyalingania

Miongoni mwa tabia na sifa ambazo anatakiwa – bali analazimika – kuwa nazo yule mlinganizi ni yeye kutendea kazi ulinganizi wake na awe ni kiigizo chema kwa yale anayolingania kwayo. Asiwe miongoni mwa wale wanaolingania katika kitu kisha yeye akakiacha au anakikataza kisha akakifanya. Hii ni hali ya waliokhasirika.

Kuhusu waumini na waliopata faida ni walinganizi wa haki ambao wanafanyia kazi ulinganizi wao, wanapata uchangamfu kwayo na wanaikimbilia. Sambamba na hayo wanajitenga mbali na yale wanayoyakataza. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِمَ تَقُولُونَ مَا لَا تَفْعَلُونَ كَبُرَ مَقْتًا عِندَ اللَّـهِ أَن تَقُولُوا مَا لَا تَفْعَلُونَ

“Enyi walioamini!  Kwanini mnasema yale msiyoyafanya? Ni chukizo kubwa kabisa mbele ya Allaah kwamba mnasema yale msiyoyafanya.”[1]

Amesema (Subhaanah) alipokuwa akiwasimanga mayahudi kwa kuwaamrisha kwao watu wema ilihali wanazisahau nafsi zao:

أَتَأْمُرُونَ النَّاسَ بِالْبِرِّ وَتَنسَوْنَ أَنفُسَكُمْ وَأَنتُمْ تَتْلُونَ الْكِتَابَ ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ

“Je, mnaamrisha watu wafanye mema na mnajisahu nafsi zenu na hali ya kuwa nyinyi mnasoma Kitabu; je, hamtii akilini?”[2]

Vilevile imesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Ataletwa mtu siku ya Qiyaamah na kuvugumizwa Motoni ambapo matumbo yake yatatoka nje. Atazunguka nayo kama punda anavozunguka kwenye kinu chake. Watu wa Motoni watakusanyika kwake na kusema: “Ee fulani! Una nini? Wewe si ulikuwa ukiamrisha mema na ukikataza maovu?” Aseme: “Nilikuwa nikikuamrisheni mema lakini mimi mwenyewe siyafanyi na nikikukatazeni maovu lakini lakini mimi mwenyewe nayafanya.”[3]

Hii ndio hali ya anayelingania kwa Allaah, akaamrisha mema na akakataza maovu halafu maneno yake yakatofautiana na matendo yake na pia matendo yakatofautiana na maneno yake.

[1] 61:02-03

[2] 02:44

[3] al-Bukhaariy (3267) na Muslim (989).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 46-47
  • Imechapishwa: 14/06/2023