Swali: Baadhi ya watu wanajisababishia wenyewe kutofunga Ramadhaan, kama vile baadhi ya vijana wanaocheza mpira wa miguu baada ya kupambazuka kwa alfajiri na hivyo wanakuwa na kiu na kulazimika kufungua. Ni ipi hukumu ya hilo?

Jibu: Nasaha zangu kwa ndugu hawa na watu mfano wao wamche Allaah (´Azza wa Jall) na wamtukuze Yeye na Shari´ah Yake. Miongoni mwa Shari´ah hizo ni pamoja na swawm. Wajiepushe kutokana na mambo yanayoharibu Shari´ah hii tukufu. Kujichosha kwa michezo na vitu vengine vya kipuuzi vinapelekea kuidhoofisha swawm na baadaye kumpelekea kulazimika kufungua, jambo ambalo ni dhambi kuu. Hata kama hatofungua mchana uliobaki atakuwa mchovu. Haya ni kinyume na vile anavotakiwa muislamu kuwa kipindi cha ´ibaadah mwenye uchangamfu na nguvu. Baadhi ya watu wanaweza kufanya yaliyo mabaya zaidi kuliko haya na wanalala mchana kutwa na wanaacha swalah, kukiwemo Dhuhr na ´Aswr, jambo ambalo ni khatari zaidi juu ya dini ya mtu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayeacha swalah ya ´Aswr basi ameyaharibu matendo yake.”[1]

Jambo ni khatari sana. Ni lazima kupupia na kutilia umuhimu maharamisho ya Allaah:

ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ حُرُمَاتِ اللَّـهِ فَهُوَ خَيْرٌ لَّهُ عِندَ رَبِّهِ

“Ndio hivyo iwe na yeyote anayetukuza vitukufu vya Allaah, basi hivyo ni kheri kwake mbele ya Mola wake.”[2]

Allaah atuwafikishe sote katika yale anayoyapenda na kuyaridhia, na atulinde sote kutokamana na yale yanayosababisha hasira Zake.

[1] al-Bukhaariy (553).

[2] 22:30

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Fataawaas-Swiyaam, uk. 30-31
  • Imechapishwa: 30/03/2022