Swali: Muadhini aliadhini ambapo tukakata swawm zetu. Baadaye ikatubainikia kuwa ameadhini dakika kadhaa kabla ya kuingia wakati. Ni kipi kinachotulazimu na ni kipi unachowanasihi waadhini?

Jibu: Muadhini akiadhini kabla ya kuzama kwa jua kimakosa na baadaye wale waliofungua wakaona kuwa ameadhini mapema, basi wanatakiwa kuilipa siku hiyo. Kwa sababu wamebainikiwa kuwa wamefungua kabla ya kuingia wakati uliowekwa katika Shari´ah, nao ni kule kuzama kwa jua. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ

“Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni swawm mpaka usiku.”[1]

Swawm zetu zinaanza na kumalizika kwa alama za wazi zinazoonekana na kila mtu. Kuanza kwa swawm ni pale kunapochomoza alfajiri na kufungua ni kwa kuzama kwa jua. Adhaana ni tangazo la kuchomoza kwa alfajiri na wakati wa Fajr na kuzama kwa jua wakati wa Maghrib. Muadhini akiadhini kimakosa, basi mnalazimika kuchunguza ili mjue kama adhaana imeafikiana na wakati au haiafikiani. Mkiacha kufanya hivo, basi mmezembea wajibu wenu na kwa ajili hiyo mtapaswa kulipa siku hiyo. Hampewi udhuru juu ya kosa la muadhini.

Kuhusiana na waadhini wanatakiwa kumcha Allaah (´Azza wa Jall) na wajitahidi kupatia wakati sahihi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Imamu ni mdhamini na muadhini ameaminiwa. Ee Allaah! Waongoze maimamu na wasamehe waadhini.”[2]

[1] 02:187

[2] Ahmad (7169), at-Tirmidhiy (207) na Abu Daawuud (517). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (237).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Fataawaas-Swiyaam, uk. 34
  • Imechapishwa: 30/03/2022