2- Mdogo. Si lazima kwake kufunga mpaka abaleghe. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kalamu imenyanyuliwa kwa watu watatu; aliyelala hadi aamke, mdogo hadi awe mkubwa na mwendawazimu hadi apate fahamu.”

Ameipokea Ahmad, Abu Daawuud, an-Nasaa´iy na al-Haakim ameisahihisha.

Lakini msimamizi wake anatakiwa kumwamrisha kufunga ikiwa anaweza kufanya hivo kwa ajili ya kumzoweza utiifu ili aizowee baada ya kubaleghe kwake kwa ajili ya kuwaigiliza as-Salaf as-Swaalih (Radhiya Allaahu ´anhum). Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walikuwa wakiwafungisha watoto wao hali ya kuwa bado wadogo na wakienda nao msikitini na wakiwatengenezea mchezo katika pamba au kitu mfano wake. Wakilia kwa ajili ya kukosa chakula basi wanawapa mchezo huo wajipumbaze kwao.

Wasimamizi na walezi wengi hii leo wanaghafilika kutokamana na jambo hilo na wala hawawaamrishi watoto wao kufunga. Bali baadhi yao wanawakatalia watoto wao kufunga pamoja na kwamba wao wenyewe wanataka. Wanadai kuwa eti ni kuwaonea huruma. Ukweli wa mambo ni kwamba kuwaonea huruma ni kule kuwasimamia watekeleze ulazima wa malezi kwa mujibu wa zile nembo za Uislamu na mafunzo yake yaliyonyooka. Yule mwenye kuwakatalia au akazembea juu ya jambo hilo basi anakuwa ni mwenye kuwadhulumu na pia mwenye kuidhulumu nafsi yake. Ni kweli kwamba wakifunga na wakaona kuwa wanadhurika kwa kufunga huko basi ni sawa hapo wakawakatalia.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 42-43
  • Imechapishwa: 21/04/2020