27. Watu wenye mapungufu makubwa katika Ramadhaan

Swali 27: Unasemaje juu ya watu wanaoshinda wanalala mchana mzima wa Ramadhaan na baadhi yao wanaswali pamoja na mkusanyiko na wengine hawaswali. Je, funga za watu hawa ni sahihi?

Jibu: Funga za watu hawa ni sahihi na zimetakasa dhimma yao. Lakini hata hivyo ni zenye mapungufu mno na zimekwenda kinyume na malengo ya Shari´ah juu ya funga. Kwa sababu Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa kufunga kama ilivyofaradhishwa kwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule asiyeacha maneno ya uongo, kuyatendea kazi na ujinga, basi Allaah hana haja kwa yeye kuacha chakula na kinywaji chake.”

Ni miongoni mwa mambo yanayotambulika kwamba kupoteza swalah na kuipuuza sio katika kumcha Allaah (´Azza wa Jall) wala kuacha kutendea kazi maneno ya uongo. Isitoshe kunaenda kinyume na makusudio ya Allaah na Mtume wake juu ya ufaradhi wa funga.

Miongoni mwa mambo ya ajabu ni kwamba watu hawa hulala mchana kutwa na wanakesha usiku mzima. Huenda hata wanakesha usiku mzima katika mambo ya upuuzi yasiyokuwa na faida kwao au katika mambo ya haramu wanayochuma kwayo madhambi.

Nasaha zangu kwa watu hawa na mfano wao wamche Allaah (´Azza wa Jall) na iwasaidie kutekeleza funga kwa njia inayomridhisha. Wanatakiwa watumie fursa ya kumtaja Allaah, kusoma Qur-aan, kuswali, kuwatendea wema viumbe na mengineyo yanayopelekewa na Shari´ah ya Kiislamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni miongoni mwa watu wenye kujitolea sana. Lakini alikuwa ni mkarimu zaidi katika Ramadhaan wakati ambapo Jibriyl anapokutana na kumsomesha Qur-aan. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni mwenye kujitolea zaidi katika mambo ya kheri kuliko upepo uliotumilizwa[2].

[1] 02:183

[2] al-Bukhaariy (1902) na Muslim (2308).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 48 mas-alatu fiy Swiyaam, uk. 26
  • Imechapishwa: 21/04/2021