Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلَوْلَا كَانَ مِنَ الْقُرُونِ مِن قَبْلِكُمْ أُولُو بَقِيَّةٍ يَنْهَوْنَ عَنِ الْفَسَادِ فِي الْأَرْضِ إِلَّا قَلِيلًا مِّمَّنْ أَنجَيْنَا مِنْهُمْ ۗ وَاتَّبَعَ الَّذِينَ ظَلَمُوا مَا أُتْرِفُوا فِيهِ وَكَانُوا مُجْرِمِينَ

“Basi kwanini hawakuweko katika karne za kabla yenu, watu weledi wanakataza ufisadi katika ardhi isipokuwa wachache kati ya Tuliowaokoa miongoni mwao! Na wale waliodhulumu wakafuata [anasa] walizostareheshwa nazo na wakawa wahalifu.” (11:116)

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu ulianza ni kitu kigeni na utarudi kuwa kitu kigeni kama ulivyoanza. Hivyo Twubaa kwa wale wageni!”[1]

Ameipokea Muslim.

Ahmad amepokea kupitia kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa:

“Ni kina nani wageni?” Akajibu: “Ni watu wachache katika makabila.”[2]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Wageni ni wale wanaotengeneza pale wanapoharibika watu.”[3]

Ahmad amepokea kupitia kwa Sa´d bin Abiy Waqqaas kwa muundo:

“Twubaa kwa wageni siku ambayo watu wameharibika!”

at-Tirmidhiy amepokea kupitia kwa Kathiyr bin ´Abdillaah, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake kwa muundo:

“Twubaa kwa wageni wenye kutengeneza yale waliyoharibu watu katika Sunnah zangu!”[4]

Abu Umayyah amesema:

“Nilimuuliza Abu Tha´labah al-Khushaniy (Radhiya Allaahu ´anh) juu ya Aayah:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا عَلَيْكُمْ أَنفُسَكُمْ ۖ لَا يَضُرُّكُم مَّن ضَلَّ إِذَا اهْتَدَيْتُمْ

“Enyi mlioamini! Ni juu yenu [majukumu ya] nafsi zenu. Hawakudhuruni waliopotoka, ikiwa mmeongoka.” (05:105)

Akajibu: “Ninaapa kwa Allaah ya kwamba mimi mwenyewe nilimuuliza nayo mtu mjuzi; nilimuuliza Mtume wa Allaah na akasema: “Mtaamrishana mema na kukatazana maovu. Pindi mnapoona choyo inayotiiwa, matamanio yanayofuatwa, dunia inayopewa kipaumbele na jinsi kila mmoja anavyopendekeza maoni yake, basi hapo shikamana na nafsi yako na uachane watu wajinga. Mbele yenu kunakuja masiku ambayo mwenye subira ni kama mfano wa aliyeshika kaa [la moto] na mtendaji mwenye kutenda kama nyinyi analipwa ujira wa wanaume khamsini.” Tukasema: “Katika sisi au katika wao?” Akasema: “Katika nyinyi.”[5]

Ameipokea Abu Daawuud na at-Tirmidhiy.

MAELEZO

Hapa kuna mashaji´isho kuwa na msimamo katika zama za ugeni na kwamba muumini anatakiwa anyooke na apupie kuwa na msimamo wakati wa ugeni wa watu. Asidanganyike na wingi wa walioangamia. Kwa ajili hii amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth wakati Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) aliposoma Aayah hii:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا عَلَيْكُمْ أَنفُسَكُمْ ۖ لَا يَضُرُّكُم مَّن ضَلَّ إِذَا اهْتَدَيْتُمْ

“Enyi mlioamini! Ni juu yenu [majukumu ya] nafsi zenu. Hawakudhuruni waliopotoka, ikiwa mmeongoka.”

Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Watu wanapoona maovu na wasiyazuie, basi Allaah anakaribia kueneza adhabu kwao wote.”[6]

Miongoni mwa uongofu ni kuamrisha mema na kukataza maovu. Watu hawadhuriki na waliopotea muda wa kuwa wao wamenyooka, wanaamrisha mema na kukataza maovu.

Baadhi ya watu wanafikiri kuwa ikiwa wameongoka maana yake ni kwamba wakitenda wao mema, basi wao hawatodhurika. Dhana ambayo ni ya kimakosa. Katika uongofu kunaingia kuamrisha mema na kukataza maovu. Kitendo hicho ni katika sababu za uongofu. as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) pindi walipopuuza aliwatolea watu Khutbah na kuwaambia:

”Hakika nyinyi mnasoma Aayah hii na kuiweka mahali pasipokuwa pake:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا عَلَيْكُمْ أَنفُسَكُمْ ۖ لَا يَضُرُّكُم مَّن ضَلَّ إِذَا اهْتَدَيْتُمْ

“Enyi mlioamini! Ni juu yenu [majukumu ya] nafsi zenu. Hawakudhuruni waliopotoka, ikiwa mmeongoka.”

Mimi nilimsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

”Watu wanapoona maovu na wasiyazuie, basi Allaah anakaribia kueneza adhabu kwao wote.”

Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoulizwa kuhusu Aayah hiyo alisema:

“Mtaamrishana mema na kukatazana maovu. Pindi mnapoona choyo inayotiiwa, matamanio yanayofuatwa, dunia inayopewa kipaumbele na jinsi kila mmoja anavyopendekeza maoni yake, basi hapo shikamana na nafsi yako na uachane watu wajinga. Mbele yenu kunakuja masiku ambayo mwenye subira ni kama mfano wa aliyeshika kaa [la moto] na mtendaji mwenye kutenda kama nyinyi analipwa ujira wa wanaume khamsini.” Tukasema: “Katika sisi au katika wao?” Akasema: “Katika nyinyi.”

[1] Muslim (145).

[2] Ahmad (1/398).

[3] Zawaa’id-ul-Musnad (4/73).

[4] at-Tirmidhiy (2630) ambaye amesema: ”Hadiyth ni Hasan na Swahiyh.”

[5] Abu Daawuud (4341), at-Tirmidhiy (3058) na Ibn Maajah (4014).

[6] at-Tirmidhiy (2168) ambaye amesema:

”Hadiyth hii ni Swahiyh.”

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Fadhwl-il-Islaam, uk. 47-50
  • Imechapishwa: 10/11/2020