119 – Ibn Fudhwayl ametuhadithia, kutoka kwa ´Atwaa’ bin as-Saa-ib, kutoka kwa Muhaarib, kutoka kwa Ibn Buraydah, ambaye ameeleza:

”Tulifika Madiynah tukamwendea ´Abdullaah bin ´Umar na kusema: ”Ee Abu ´Abdir-Rahmaan! Tunasafiri ardhini na tunakutana na watu wanaosema ya kwamba hakuna makadirio.” Akasema: ”Je, ni katika waislamu wanaoswali kuelekea Qiblah?” Tukasema: ”Ndio,  ni katika wanaoswali kuelekea Qiblah.” Akaghadhibika sana kiasi cha kwamba nikatamani nisingemuuliza. Kisha akasema: ”Ukikutana nao, basi waeleze kuwa ´Abdullaah bin ´Umar hana chochote kuhusiana nao na wao hawana chochote kuhusiana nami. Ukipenda basi nitakweleza kuhusu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Nikasema: ”Ndio.” Akasema: ”Wakati tulipokuwa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tahamaki alikuja bwana mmoja aliyekuwa amevalia vizuri, anayenukia vizuri na mwenye uso mzuri na akasema: ”Ee Mtume wa Allaah, Uislamu ni nini?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan, kuhiji Nyumba na kuoga kutokana na janaba.” Akasema: ”Umesema kweli.” Kisha akasema: ”Ee Mtume wa Allaah, imani ni kitu gani?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Kumwamini Allaah, siku ya Mwisho, Malaika Wake, Vitabu, Mitume na makadirio, ya kheri na shari yake, matamu na machungu.” Akasema: ”Umesema kweli.” Halafu akaondoka zake. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Nileteeni bwana yule!” Tukaenda sote kumtafuta, lakini hatukumpata. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Huyu ni Jibriyl (´alayhis-Salaam) aliyekuja kukufunzeni dini yenu.”[1]

120 – Ibn Mahdiy ametuhadithia, kutoka kwa Sufyaan, kutoka kwa Abu Ishaaq, kutoka kwa Abu Laylaa[2] al-Kindiy, kutoka kwa Hujr bin ´Adiy, ambaye ameeleza kuwa ´Aliy amewaeleza na kusema:

”Usafi ni nusu ya imani.”

121 – ´Affaan ametuhadithia: Abaan al-´Attwaar ametueleza: Yahyaa bin Abiy Kathiyr ametueleza, kutoka kwa Zayd Abu Salaam, kutoka kwa Abu Maalik al-Ash´ariy, ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Usafi ni nusu ya imani.”

[1] Swahiyh. Hata hivyo Muslim ameipokea kupitia njia nyingine kutoka kwa Buraydah, kutoka kwa Yahyaa bin Ya´mar, kutoka kwa Ibn ´Umar, pasi na kutaja josho la janaba. Lakini josho likapokelewa kupitia njia nyingine kutoka kwa Yahyaa bin Ya´mar kwa Ibn Khuzaymah, na kupitia kwake kwa Ibn Hibbaan (16) na ad-Daaraqutwniy (282), aliyesema kuwa cheni ya wapokezi imethibiti na ni Swahiyh. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea mfano wake kutoka kwa Abu Hurayrah.

[2] Imekuja katika ile ya asili ”Ibn Abiy Laylaa”. Masahihisho yamefanywa baada ya ”al-Muswannaf” na vitabu vya nyasifu. Cheni ya wapokezi kwenda mpaka kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) ni dhaifu, lakini Hadiyth ni Swahiyh kwa njia ya maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ameipokea Muslim na wengineo, kupitia kwa Abu Maalik al-Ash´ariy. Inakuja baada yake.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 44-45
  • Imechapishwa: 17/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy