Wakati Allaah (´Azza wa Jall) anapokiita kitu kimoja kwa majina mawili au matatu, vimeungana na si vyenye kutengana. Na anapoviita vitu viwili kwa majina mawili yanayotofautiana, ameviunganisha. Kwa mfano aliposema (Ta´ala):

قَالُوا يَا أَيُّهَا الْعَزِيزُ إِنَّ لَهُ أَبًا شَيْخًا كَبِيرًا

“Wakasema: “Ee waziri! Hakika yeye ana baba mkongwe.”[1]

Amekiita kitu kimoja kwa majina matatu (أَبًا شَيْخًا كَبِيرًا), jambo linalofahamisha kuwa ni kitu kimoja na ni hichohicho. Hakusema kuwa ni baba, mzee na mtumzima (أَبًا شَيْخًا كَبِيرًا). Amesema (Ta´ala):

عَسَىٰ رَبُّهُ إِن طَلَّقَكُنَّ أَن يُبْدِلَهُ أَزْوَاجًا خَيْرًا مِّنكُنَّ مُسْلِمَاتٍ مُّؤْمِنَاتٍ قَانِتَاتٍ تَائِبَاتٍ عَابِدَاتٍ سَائِحَاتٍ ثَيِّبَاتٍ وَأَبْكَارًا

“Akikutalikini, basi wajibu kwa Mola Wake kumbadilishia wake bora kuliko nyinyi; waislamu, waumini, watiifu na wanyenyekevu, wanaotubia, wafanya ‘ibaadah, wafungao na wanaohajiri, wajane na mabikra.”[2]

Ilipokuwa wanawake waliokwishaolewa sio bikira, akatenganisha maneno hayo mawili na kusema:

وَأَبْكَارًا

”… na mabikira.”

Amesema tena:

وَمَا يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ

”Halingani sawa kipofu na mwenye kuona.”[3]

Ilipokuwa mwenye kuona sio kipofu, akayatenganisha. Kisha amesema (Ta´ala):

وَلَا الظُّلُمَاتُ وَلَا النُّورُ وَلَا الظِّلُّ وَلَا الْحَرُورُ

”… wala viza na nuru, wala kivuli na joto.”[4]

Ilipokuwa kila kimoja katika vilivyotajwa kinatofautiana na kingine, akavitenganisha. Kisha  amesema:

هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ ۖ هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ الْعَزِيزُ الْجَبَّارُ الْمُتَكَبِّرُ ۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يُشْرِكُونَ هُوَ اللَّـهُ الْخَالِقُ الْبَارِئُ الْمُصَوِّرُ

”Yeye ni Allaah, ambaye hakuna mungu wa haki isipokuwa Yeye, mjuzi wa yaliyofichikana na ya dhahiri, Yeye ni Mwenye kurehemu. Yeye ni Allaah, ambaye hakuna mungu wa haki isipokuwa Yeye, mfalme, mtakatifu, Mwenye kusalimisha na kusalimika, Mwenye kusadikisha ahadi na kuaminisha, Mwenye kudhibiti, kushuhudia, kuchunga na kuhifadhi, Mwenye nguvu zisizoshindwa, Jabari, Mwenye ukubwa na utukufu – Utakasifu ni wa Allaah kutokamana na ambayo wanamshirikisha. Yeye ni Allaah, muumbaji, mwanzishi viumbe, muundaji sura.”[5]

Majina yote ni ya kitu kimoja. Majina yameungana na si yenye kutengana. Kwa ajili hiyo wakati Allaah anaposema:

أَلَا لَهُ الْخَلْقُ وَالْأَمْرُ

”Tanabahi! Ni Vyake pekee uumbaji na amri.”[6]

Kwa sababu viumbe sio amri, maneno hayo mawili ni yenye kutofautiana[7].

[1] 12:78

[2] 66:5

[3] 35:19

[4] 35:20-21

[5] 59:23-24

[6] 7:54

[7] Ibn ´Aqiyl al-Hanbaliy amesema:

”Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ameandika kitabu kinachoitwa ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah wal-Qadariyyah.” (al-Aadaab ash-Shar´iyyah (1/274))

Ibn Taymiyyah amesema:

”Kama alivosema Imaam Ahmad katika kitabu chake ”ar-Radd ´alaaz-Zanaadiqah wal-Jahmiyyah.”  (Tafsiyr Suurat-il-Ikhlaasw, uk. 239)

Ibn Kathiyr amesema:

”… na hivo ndivo alivosema Ahmad bin Hanbal katika kitabu ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah” (Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (3/304))

Ibn Hajar al-´Asqalaaniy amesema:

”Amesema waziwazi Ahmad katika kitabu “ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah.” (Fath-ul-Baariy (13/598))

  • Mhusika: Imaam Ahmad bin Hanbal (afk. 241)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 108-110
  • Imechapishwa: 22/04/2024