27. Ni ipi hukumu ya kuosha mguu wa kulia na kisha kuuvisha soksi?

Swali 27: Ni ipi hukumu ya ambaye ametawadha ambapo akaosha mguu wake wa kulia kisha akavaa soksi za ngozi au soksi za kawaida na baada ya hapo akaosha mguu wa kushoto na akavaa soksi za kawaida au soksi za ngozi?

Jibu: Wanazuoni wametofautiana juu ya jambo hili. Wako wanazuoni waliosema kuwa ni lazima akamilishe twahara kabla ya kuzivaa. Wengine wakasema akiosha mguu wa kulia basi inafaa kwake kuvaa soksi za ngozi au soksi za kawaida halafu baada ya hapo akaosha mguu wa kushoto na akavaa soksi za ngozi au soksi za kawaida. Huyu hakuvaa soksi za kuliani wala soksi za kushotoni isipokuwa baada ya kusafisha mguu. Kwa maana nyingine ni kwamba amezivaa akiwa na twahara. Lakini ipo Hadiyth iliopokelewa na ad-Daaraqutwniy na al-Haakim ambaye ameisahihisha ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anapotawadha mmoja wenu na akavaa soksi zake za ngozi… “

Maneno yake “Anapotawadha mmoja wenu… “ yanaweza kuyapa nguvu yale maoni ya kwanza. Kwa sababu ambaye hajaosha mguu wa kushoto hazingatiwi kuwa ameshatawadha. Kwa ajili hiyo bora ni kutendea kazi maoni hayo.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Buhuuth wa Fataawaa fiyl-Mas´h ´alaal-Khuffayn, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (11/175)
  • Imechapishwa: 06/05/2021