27. Mwanamke anatumia vidonge vya kuzuia hedhi ili aweze kufunga Ramadhaan

Swali: Ni ipi hukumu ya mwanamke kutumia vidonge vinavyozuia ada ya mwezi katika mwezi wa Ramadhaan ili aweze kuswali na kufunga pamoja na wengine?

Jibu: Ikiwa mwanamke anataka kutumia vidonge vinavyozuia hedhi na ujauzito, basi yapo mambo ambayo anapaswa kuyaangalia. Isitoshe analazimika kuwataka ushauri wale madaktari wabobezi ili kujua kama vidonge hivyo vinaendana naye au vinamdhuru. Ikiwa vinamdhuru basi haijuzu kwake kuvitumia. Na ikiwa havimdhuru basi kutaulizwa kama kule kuvitumia ni jambo limewekwa katika Shari´ah au halikuwekwa katika Shari´ah. Ikiwa havihitajii au ni kutokana na sababu ambayo haikuwekwa katika Shari´ah, kama kukata kizazi, basi haitojuzu kwake kuvitumia. Na ikiwa ni kutokana na sababu inayokubalika katika Shari´ah, kama kupangilia kizazi au kuhiji, basi kutaulizwa kama mume wake ameidhinisha jambo hilo au hakuliidhinisha. Akimpa idhini ya kuvitumia, basi anaruhusiwa kuvitumia na vinginevyo hatoruhusiwa.

Pamoja na haya yote haitakikani kwa wanawake kujizoweza na kujiingiza katika madawa haya. Kwa sababu imetuthibitikia kwamba tembe kama hizi zinasababisha kukorogeka kwa ada ya mwezi ambapo kiasi kikubwa cha maisha yake kinakuwa katika mkorogeko, khaswa ´ibaadah kama ya swalah, swawm na hajj. Kwa ajili hiyo mimi namnasihi mwanamke kutotumia vidonge hivyo na kuyaacha mambo juu ya maumbile yake kama Allaah alivyoyaumba. Hakika Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) ni Mwingi wa hekima zaidi kuliko wenye hekima wote na Mjuzi wa mambo yote, kukiwemo yale yanayosilihi kwa waja Wake. Kwa ajili hiyo haitakikani kwake kujiingiza katika mambo haya yanayosababisha kuchanganyika na kukorogeka kwa ada yake na baadaye ´ibaadah zake. Wanawake wa kiswahabah (Radhiya Allaahu ´anhunna) wote ilikuwa inapowajia hedhi katika Ramadhaan, basi wanaacha kufunga na baadaye wanalipa masiku yao. Jambo limewepesishwa. Wakati mwanamke anapata ada yake ya mwezi, kisha baadaye analipa zile siku alizokula baada ya Ramadhaan. Hakika yuko na kiigizo chema kwa wanawake wa kiswahabah (Radhiya Allaahu ´anhunna). Mama wa waumini (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Nilikuwa nadaiwa swawm ya Ramadhaan na nashindwa kulipa mpaka katika Sha´baan. Hayo ni kutokana na nafasi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwangu.”[1]

Wigo ni mpana katika jambo hili. Mwanamke hahitajii kutumia vidonge hivi vinavyosababisha mkorogeko.

[1] al-Bukhaariy na Muslim.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah Aalush-Shaykh
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Fataawaas-Swiyaam, uk. 29-30
  • Imechapishwa: 28/03/2022