Kuhusiana na vifaa vya kuchezea ambavyo vina picha ya vitu vyenye roho ni jambo ambalo wanazuoni wametofautiana juu ya kufaa kwake kwa watoto wa kike kuvitumia. Imethibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim ya kwamba ´Aaishah amesema:

“Nilikuwa nikicheza doli za wasichana wangu kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nilikuwa na marafiki zangu wa kike wakicheza pamoja nami. Ilikuwa wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapoingia, basi wanapotea. Huwaacha wakacheza nami.”[1]

Haafidhw [Ibn Hajar] amesema:

“Baadhi ya watu wametumia Hadiyth hii kama dalili juu ya kufaa kwa wasichana kucheza na doli na vitu vya kuchezea ili wavitumie kama mchezo. Hadiyth hii imefanya maalum yale makatazo ya picha yaliyokuja kwa njia ya kuenea. al-Qaadhwiy ´Iyaadhw ameyathibitisha na akasema kuwa kikosi cha wanazuoni wengi wana maoni haya. Wanaonelea kuwa inafaa kuwauzia wasichana michezo hii ili kuwazoweza tangu utotoni mwao kusimamia mambo ya nyumba zao na watoto wao. Amesema kuwa baadhi yao wamesema kuwa imefutwa. Hayo ni maoni ya Ibn Battwaal. Ibn Abiy Zayd amesimulia kutoka kwa Maalik ambaye amesema kuwa imechukizwa kwa baba kumnunulia mtoto wake wa kike picha. Kutokana na hayo ad-Daawuudiy amesema kuwa suala hio limefutwa.

Ibn Hibbaan ameandika katika kitabu chake kichwa cha khabari kinachosema:

“Kufaa kwa wasichana wadogo kucheza michezo.”

an-Nasaa´iy pia amefanya hivo na kusema:

“Kufaa kwa mwanamme kumwacha mke wake kucheza na doli.”

Hata hivyo hakulifungamanisha na mke mdogo, jambo ambalo lina walakini.

al-Bayhaqiy amesema baada ya kuitoa Hadiyth hii:

“Yamethibiti makatazo ya picha. Kwa hiyo maana yake ni kwamba ruhusa kwa ´Aaishah ilikuwa kabla ya kuharamishwa.”

Haya ndio maoni ya Ibn-ul-Jawziy.”

Abu Daawuud na an-Nasaa´iy wamepokea kupitia njia nyingine kutoka kwa ´Aiashah ambaye amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alirudi kutoka katika vita vya Tabuuk au vya Khaybar. Chumbani kwake kulikuwa pazia. Upepo ukapeperusha ncha ya pazia iliokuwa imefunika watoto wa sanamu aliokuwa akichezea ´Aaishah. Akasema: “Nini hii, ee ´Aaishah?” Akasema: “Ni watoto wangu wa kike.” Kati yao aliona farasi mwenye mbawa mbili aliyetengenezwa kwa kitambaa. Akasema: “Ni nini hiki ninachoona katikati yao?” Akajibu: “Ni farasi.” Akasema: “Ni nini hivyo vilivyo juu yake?” Akasema: “Ni mbawa mbili.” Akasema: “Farasi mwenye mbawa mbili?” Akajibu: “Je, wewe hukusikia kuwa Sulaymaan alikuwa na farasi aliye na mbawa?” ´Aaishah anaendelea kusimulia: “Basi akacheka (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka nikaona magego yake.”[2]

al-Khattwaabiy amesema:

“Katika Hadiyth hii tunapata faida kwamba kucheza kwa doli sio kama kucheza na picha nyenginezo ambazo kumepokelewa matishio juu yake. Alimruhusu ´Aaishah kufanya hivo kwa sababu kipindi hicho alikuwa bado hajalabeghe.”

Kusema kwa kukata namna hiyo ni jambo lina walakini. Lakini kuna uwezekano ikawa hivo. Kwani ´Aaishah katika vita vya Khaybar alikuwa ni msichana wa miaka kumi na minne. Ima alikuwa ameikamilisha, ameivuka au ameikaribia. Lakini katika vita vya Tabuuk alikuwa amekwishabaleghe kabisa. Kwa hivyo unapata nguvu upokezi uliosema kwamba ilikuwa ni Khaybar. Yanaoanishwa kwa yale aliyosema al-Khattwaabiy. Kufanya hivo ni bora kuliko kugonganisha.”[3]

Ukishatambua aliyosema Haafidhw (Rahimahu Allaah), basi lililo la tahadhari zaidi ni kuepuka vitu vya kuchezea vilivyo na picha. Kuna uwezekano Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwacha ´Aaishah achezee doli kabla ya makatazo. Katika hali hiyo, kitendo hicho kitakuwa kimefutwa kwa zile Hadiyth zinazoamrisha kufuta na kuharibu picha isipokuwa ile iliyokatwa kichwa chake au ikawa yenye kutwezwa kama alivyoonelea al-Bayhaqiy na Ibn-ul-Jawziy na akamili katika maoni hayo Ibn Battwaal. Kuna uwezekano vilevile hali hiyo ni maalum, kama wanavoonelea wanazuoni wengi, kwa ajili ya manufaa ya kuwapa mazoezi wasichana. Isitoshe kule watoto wa kike kucheza navyo ni aina fulani ya kuvitweza. Licha ya uwezekano uliotajwa na shaka ya kufaa kwake tahadhari zaidi itakuwa kuviepuka. Watoto wa kike wapewe mazoezi ya vitu vya kuchezea visivyokuwa doli kwa ajili ya kukata suala la kubaki kwa picha zenye viwiliwili na pia kutendea kazi maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Achana na kile chenye kukutia shaka na kiendeee kisichokutia shaka.”[4]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa an-Nu´maan bin Bashiyr ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Halali iko wazi na haramu iko wazi na kati ya mawili hayo mna yenye kutia shaka. Wengi miongoni mwa watu hawayajui. Hivyo basi, yeyote atakayejiepusha yenye kutia shaka, basi atakuwa amejiepushia shaka katika dini yake na heshima yake. Na yeyote atakayetumbukia katika yenye kutia shaka, basi ataingia ndani ya haramu. Kama mchunga anayechunga kando ya mipaka, ni haraka kulisha humo.”[5]

Allaah ndiye mjuzi zaidi.

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhamamd na kizazi chake.

[1] al-Bukhaariy (6130) na Muslim (2440).

[2] Abu Daawuud (4932).

[3] Fath-ul-Baariy.

[4] at-Tirmidhiy (2518), an-Nasaa´iy (5711), Ahmad (01/200) na ad-Daarimiy (2532).

[5] al-Bukhaariy (52), Muslim (1599), at-Tirmidhiy (1205), an-Nasaa´iy (4453), Abu Daawuud (3329), Ibn Maajah (3984), Ahmad (04/270) na ad-Daarimiy (2531).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Jawaab al-Mufiyd fiy Hukm-it-Taswwiyr kutoka katika Majmuu´-ul-Fataawaa (04/221-222)
  • Imechapishwa: 28/03/2022