27. Makafiri wajinga walielewa malengo ya Mtume kuwaambia watamke Shahaadah tofauti na hawa wa leo

Makafiri wajinga walijua kuwa anachokusudia Mtume (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) kwa neno hili ni kumpwekesha Allaah (Ta´ala) kwa ´Ibaadah na kukanusha vyote vinavyoabudiwa badala Yake na kujiweka navyo mbali kabisa. Hakika wakati alipowaambia waseme “hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah”, walisema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عُجَابٌ

“Amewafanya miungu wote kuwa ni mungu mmoja? Hakika hili ni jambo la ajabu mno.” (Swaad 38 : 05)

MAELEZO

Makafiri walijua maana ya ´hapana mungu isipokuwa Allaah` na kwa ajili hii ndio maana pindi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaambia:

“Semeni ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah`.” Ahmad (03/492).

Walisema:

أَجَعَلَ الْآلِهَةَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا

“Amewafanya waungu wote kuwa ni mungu Mmoja?” (38:05)

Pindi vilevile alipowaambia:

“Semeni ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah`.” Ahmad (03/492).

Walisema:

أَئِنَّا لَتَارِكُو آلِهَتِنَا لِشَاعِرٍ مَّجْنُونٍ بَلْ جَاءَ بِالْحَقِّ وَصَدَّقَ الْمُرْسَلِينَ

“Je, hivi kweli sisi tuache miungu yetu kwa ajili ya mshairi mwendawazimu? Bali amekuja kwa haki na amewasadikisha Mitume.” (37:36-37)

Walifahamu maana ya ´hapana mungu isipokuwa Allaah` na hivyo wakakataa kuitambua kwa kuwa inawalazimu kuacha kuyaabudu masanamu, jambo ambalo walikuwa hawataki. Walichokuwa wanataka ni kubaki katika kuyaabudu masanamu. Hawakuthubutu kusema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` na wakabaki kuyaabudu masanamu kwa kuwa katika haya kuna kujigonga na wao wanakimbia kutokamana na kujigonga ilihali leo kuna wengi wanaojinasibisha na Uislamu hawaogopi kujigonga huku. Utawakuta wanasema ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` kwa herufi na wakati huo huo wanaenda kinyume nayo na wanamuabudu asiyekuwa Allaah katika makaburi, waja wema, miti, mawe na vinginevyo. Hawafahamu maana ya ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah`. Haitoshi kutamka ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` pasi na kutambua maana yake na kutendea kazi yale inayopelekea. Ni lazima kwa mtu atambue maana yake halafu atendee kazi yale inayopelekea. Kwa kuwa haiwezekani mtu akatendea kazi maana yake na yale inayopelekea ilihali mtu anajahili maana yake. Ndio maana anasema (Jalla wa ´Alaa):

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ

“Basi jua ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako na kwa ajili ya waumini wa kiume na waumini wa kike.” (47:19)

Ameanza kwa elimu kabla ya kuzungumza na kutenda. Asiyejua maana ya ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah` hawezi kutendea kazi yale inayopelekea kwa njia sahihi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 43
  • Imechapishwa: 10/11/2016