27. Majibu kwa njia nyingi kuonyesha kwamba mtu anaweza kukufuru hata kama ametimiza nguzo za Uislamu III

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Yaweza kusemwa pia: “Banuu ´Ubayd al-Qaddaah, waliokuwa wakimiliki Magharibi [ya Afrika] na Misri katika zama za Banuu al-´Abbaas, wote walikuwa wakishuhudia ya kuwa hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Walikuwa wanadai Uislamu, wanaswali ijumaa na swalah za mikusanyiko. Ilipodhihiri kukhalifu kwao Shari´ah katika mambo fulani ambayo sisi hatuyafuati, walikubaliana wanachuoni kuwa ni makafiri na kwamba inatakiwa kuwapiga vita na kwamba miji yao ni miji ya vita. Hivyo Waislamu wakawashambulia mpaka wakaokoa waliokuwa nayo katika miji ya Waislamu.

Yaweza kusemwa pia: “Ikiwa watu wa mwanzo hawakukufuru, isipokuwa kwa kujumuisha kwao baina ya shirki na kumkadhibisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Qur-aan na kupinga kufufuliwa na kadhalika, ni nini maana ya mlango uliotajwa na wanachuoni wa kila madhehebu “Mlango: Hukumu ya mwenye kuritadi”, naye ni yule Muislamu ambaye anakufuru baada ya Uislamu wake? Halafu wakataja aina nyingi; kila aina inakufurisha na kuhalalisha damu ya mtu na mali yake. Mpaka walitaja mambo ambayo yalionekana ni madogo kwa yule mwenye kuyafanya, kama mfano maneno yaliosemwa na mdomo wake bila ya kuyamaanisha moyoni mwake au maneno aliyosema kwa njia ya mzaha na mchezo.

MAELEZO

Ukaguzi huu ni Radd dhidi ya waabudu makaburi na waabudu mawalii katika zama za mtunzi wa kitabu kama ilivyotangulia. Shaykh (Rahimahu Allaah) anasimamisha hoja dhidi yao. Kwa sababu mtu anapofanya kitu chenye kukufurisha anakufuru. Haijalishi kitu hata kama atashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Kwa sababu wanatumia hoja dhidi yao eti makafiri wa Quraysh na mfano hao hawashuhudii ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah na eti kwamba wao wanashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, wanaswali na wanafunga. Wanauliza ni vipi tutatumia hoja dhidi yao kwa Aayah zilizoshuka juu ya makafiri wa Quraysh. Wanasema kuwa makafiri wa Quraysh wanaabudu masanamu na hawashuhudii ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Vilevile wanasema kuwa walikadhibisha na wakapambana. Wanasema kuwa wao si kama wale. Mtunzi wa kitabu akatumia hoja nyingi zinazobainisha ukafiri wao hata kama wanashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah. Ni kama ambavyo wanafiki wanashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, wanaswali na wanafunga. Pamoja na haya wao ni makafiri zaidi ya watu na watakuwa kwenye tabaka ya chini kabisa Motoni. Kwa sababu wamesema kwa ndimi zao yasiyokuwemo mioyoni mwao. Wanasema ´hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah` na kwa ndani wanayakadhibisha. Vivyo hivyo waislamu wamewakadhibisha mayahudi ilihali ni wenye kusema ´hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah`. Kadhalika wale washirikina ambao wamemwabudu ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh), wakamuomba uokozi, wakaliabudu jua, mwezi na vyenginevyo. Kwa sababu wamefanya mungu mwengine pamoja na Allaah. Haijalishi kitu japokuwa wataswali na wakafunga. Wakati walipodhihirisha madhehebu ya Raafidhwah, kuchupa mipaka kwa watu wa nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), baadhi yao wakadai kuwa ndiye mungu na kwamba ana haki ya kuabudiwa badala ya Allaah, ndipo waislamu waliwakufurisha na wakawapiga vita kwa sababu ya kudhihirisha kwao ukafiri na upotevu. Hakukuwanufaisha kitu kushuhudia kwao kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah. Hayo ni kutokana na ukafiri wao, upotofu wao, kuchupa kwao mipaka kwa watu wa familia ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kudai uungu juu ya wale wakuu wao. Jengine ni kwa sababu wameabudu badala ya Allaah na kuziweka nafsi zao nafasi za uungu. Matokeo yake waislamu wakawakufurisha na wakawapiga vita kwa sababu ya ukafiri wao. Hakukuwafaa kitu kushuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah midhali wamefanya mambo yenye kukufurisha.

Maimamu katika madhehebu yote (Hanaabilah, ash-Shaafi´iyyah, Maalikiyyah na Hanafiyyah) wametunga mlango kwa jina “Hukumu ya mwenye kuritadi”. Ni mlango maarufu ambao waislamu wamekubaliana. Wamefanya hivo kwa kutendea kazi maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kubadilisha dini yake muueni.”[1]

Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh) amesema kuhusu mwenye kuibadilisha dini yake:

“Hukumu ya Allaah na Mtume Wake.”

Hapa ilikuwa pale ambapo myahudi aliposilimu kisha akaritadi. Ndipo Mu´aadh akaenda kwa Abu Muusa na myahudi huyo alikuwa hapo akimwambia alete tawbah. Mu´aadh akamwambia:

“Siteremki mpaka auawe. Hiyo ni hukumu ya Allaah na Mtume Wake.”

Kwa sababu amebadilisha dini yake.

Vivyo hivyo mwenye kuukubali Uislamu kisha akafanya kitu chenye kukufurisha. Wanachuoni (Rahimahumu Allaah) wamebainisha kwenye mlango unaozungumzia kuhusu kuritadi ya kwamba anakufuru. Haijalishi kitu hata kama anaswali na anafunga. Haijalishi kitu hata kama anashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Kwa mfano kuna mtu anaswali na anafunga. Kisha baada ya hapo akamtukana Allaah na Mtume Wake anakufuru japokuwa anaswali na anafunga. Iwapo atasema kuwa swawm sio lazima anakufuru. Iwapo atasema kuwa swalah sio lazima anakufuru. Endapo atasema kuwa uzinzi ni halali anakufuru. Iwapo atasema kuwa pombe ni halali anakufuru. Haijalishi kitu hata kama anaswali, anafunga na anashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah. Mwenye kuukanyaga msahafu kwa miguu yake na akautupa kwenye mkojo hali ya kuutweza anakufuru. Akisema kuwa ni halali kumuoa mama, dada au mtu akamuoa msichana wake anakufuru kwa matendo hayo. Haijalishi kitu hata kama anashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhamamd ni Mtume wa Allaah. Kadhalika walimwambia akifungamana na asiyekuwa Allaah na akaliabudu jua, mwezi, sanamu, ´Aliy, al-Husayn, Faatwimah, ´Abdul-Qaadir, al-Badawiy au wengineo. Ni mamoja akawa anaswali, anafunga na anashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhamamd ni Mtume wa Allaah.

[1] al-Bukhaariy (2016).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 95-97
  • Imechapishwa: 25/10/2021