Nadb ina maana ya mtu kulia kwa ajili ya maiti na kutaja mazuri yake. Yamesemwa na al-Jawhariy. Imesemekana vilevile ya kwamba maana yake ni kutaja sifa nzuri za yule maiti. Niyaahah, al-Qaadhwiy ´Iyaadhw amesema, ni wanawake kukusanyika kwa ajili ya kumlilia maiti. Katika “al-Mughniy” mna ya kwamba maana yake ni kutaja sifa nzuri za yule maiti kwa njia ya kelele.

Tambua – Allaah akurehemu – ya kwamba kinachotakikana wakati wa msiba ni kutulia, kuwa na subira na kuridhia aliyopanga Allaah (Ta´ala). Kisha inatakiwa kushukuru na kusema ” Sisi ni wa Allaah na Kwake ndiko tutarejea”, kumpa swadaqah yule msibiwaji na kumuombea du´aa. Ama Nadb, Niyaahah, kuchana nguo, kujipiga mashavu na kuzungumza maneno mabaya, yote haya yanapingana na tuliyoyataja.

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema kuwa Nadb na Niyaahah ni haramu. Katika moja ya upokezi wa Hanbal imepokelewa kuwa Niyaahah ni dhambi.

Watu wa ash-Shaafi´iy na wengine wamesema kuwa Niyaahah ni haramu.

Ibn ´Abdil-Barr amesema:

“Wanachuoni wamekubaliana juu ya kwamba Niyaahah haijuzu kwa wanaume na wanawake.”

Abul-Khattwaab (Rahimahu Allaah) amesema katika “al-Hidaayah”:

Nadb na Niyaahah imechukizwa na kuhuzunika usoni, kuchana nguo na kutembea miguu peku.”

Maoni haya ni dhaifu kwani yanapingana na yaliyotajwa katika Sunnah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 47
  • Imechapishwa: 14/10/2016