26. Kuhuzunika na kusikitika hakuna faida yoyote

Si Allaah (Ta´ala) wala Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawakuamrisha huzuni sawa katika mnasaba wa msiba wala kitu kingine. Uhakika wa mambo Allaah amekataza hilo katika Kitabu Chake hata kama utahusiana na dini. Hata hivyo kuna huzuni wenye kusifiwa na uliosemwa vibaya. Kwa mfano maneno Yake (Ta´ala):

وَلَا تَهِنُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَنتُمُ الْأَعْلَوْنَ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Na wala msilegee na wala msihuzunike na ilhali nyinyi ndio mko juu mkiwa kweli ni waumini.” 03:139

وَلَا تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ وَلَا تَكُ فِي ضَيْقٍ مِّمَّا يَمْكُرُونَ

“Na wala usiwahuzunukie na wala usiwe katika dhiki kutokana na njama wanazozifanya.” 16:127

Amesema (Ta´ala) kuhusu Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Abu Bakr:

إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّـهَ مَعَنَا

“Alipomwambia swahibu yake: “Usihuzunike – hakika Allaah Yu Pamoja nasi.” 09:40

Amesema (Ta´ala) vilevile:

فَلَا يَحْزُنكَ قَوْلُهُمْ

“Basi isikuhuzunishe kwa maneno yao.” 36:76

Yote haya kwa sababu mahuzuniko hayaleti manufaa na wala hayazuii madhara yoyote. Kwa hivyo hayana faida yoyote. Allaah haamrishi kitu kisichokuwa na faida yoyote. Pamoja na hivyo muhuzunikaji hapata dhambi midhali mahuzuniko yake hayakufungamana na kitu cha haramu tulichotaja. Kwa vile Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah haadhibu kwa machozi ya macho au kwa huzuni wa moyo. Anaadhibu au kurehemu kwa hichi” na akaashiria ulimi.”

Hii ni dalili inayofahamisha kuwa huzuni sio dhambi maadamu haukufungamana na dhambi. Linatiliwa nguvu vilevile na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika macho hutokwa na machozi na moyo huingiwa na huzuni na wala hatusemi isipokuwa yale yenye kumridhisha Mola wetu.”

Maalik bin Diynaar amesema:

“Ikiwa huzuni unakosekana kwenye moyo basi unaharibika kama nyumba iliotupu.”

´Abdullaah bin Ahmad bin Ahmad amepokea kwamba Ibraahiym bin ´Iysaa amesema:

“Sijaona mtu mwenye kuhuzunika kwa muda mrefu kama al-Hasan al-Baswriy. Kila nilipokuwa ninamwona hufikiria kuwa ametoka kupatwa na msiba.”

Baada ya hapo akataja maneno kutoka kwa Maalik aliyesema:

“Kadri na jinsi utavyohuzunika sana juu ya kitu cha kidunia ndio jinsi hupotea furaha kiasi chake kwa ajili ya Aakhirah kwenye moyo wako.”

Dalili nyingine yenye kuonesha kuwa huzuni umeruhusiwa ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا أَسَفَىٰ عَلَىٰ يُوسُفَ وَابْيَضَّتْ عَيْنَاهُ مِنَ الْحُزْنِ فَهُوَ كَظِيمٌ

“Na akajitenga nao na akasema: “Ee majonzi yangu juu ya Yuusuf!” na macho yake yakageuka meupe [kwa kulia] kutokana na huzuni naye huku akiwa amezuia ghaidhi.” 12:84

Dalili zote hizi zinafahamisha kuwa muhuzunikaji hapati dhambi. Ni sawa kulia baada na kumuhuzunikia yule aliyefariki kutokana na huruma na kumfikiria. Ni jambo lisilopingana kabisa na kuridhia na kuwa na subira tofauti na kulia na kuhuzunika kwa sababu ya maslahi ya kibinafsi. Pamoja na hivyo endapo kulia kutakuwa kumefungamana na kitu chenye kusifika ambacho muhuzunikaji analipwa kwacho, basi ni mwenye kusifika kwa mtazamo mwingine na sio kwa sababu ya huzuni kwa dhati yake. Mtu mwenye kumuhuzunikia aliyesibiwa katika dini yake na misiba ya waislamu kwa jumla basi analipwa kwa kuwatamania kwake kheri na kuchukia juu yao shari na matokeo yake.

Lakini endapo huzuni huu utachangia ile subira na mapambano yaliyoamrishwa, ule wema unaoletwa na ile shari inayozuiwa kubaki, basi kuhuzunika kutakuwa ni haramu. Katika hali hii mtu atakuwa ni mwenye kupata dhambi kwa mtazamo mwingine.

Ikiwa kile ambacho mtu anakihuzunikia hakiwezi kurudisha kile kilichokosekana, basi huzuni utakuwa hauna maana yoyote. Mwerevu hujikinga dhidi ya huzuni na kuhakikisha hajijengei huzuni baada ya huzuni. Anatambua kuwa yatakwisha baada ya muda na Allaah ndiye anajua zaidi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 45-46
  • Imechapishwa: 14/10/2016