29. Maiti huadhibiwa kwa maombolezo ya walio hai

´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Maiti anaadhibiwa ndani ya kaburi lake kwa kufanyiwa maombolezo.”

Katika upokezi mwingime imekuja:

“Maiti anaadhibiwa kwa kufanyiwa maombolezo.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

al-Mughiyrah bin Shu´bah ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimtuma mjumbe na ujumbe ufuatao:

“Yule ambaye kunafanywa maombolezo kwa ajili yake anaadhibiwa kwa kile anachoombolezewa kwacho.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Usayd bin Abiy Usayd ameeleza kupitia kwa Muusa bin Abiy Muusa ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Maiti anaadhibiwa kwa kilio cha aliye hai. Akisema: “Wewe ambaye ulikuwa ukinipa nguvu! Wewe uliyekuwa ukinisaidia! Wewe uliyekuwa ukiniruzuku!” basi anachukuliwa yule maiti na kuambiwa: “Ni kweli ulikuwa ukimpa nguvu?” Ni kweli ulikuwa ukimsaidia? Ni kweli ulikuwa ukimpa rizki?” Ndipo nikasema: “Ametakasika Allaah kutokana na mapungufu na kasoro! Kwani Allaah (Ta´ala) anasema:

وَلَا تَزِرُ وَازِرَةٌ وِزْرَ أُخْرَىٰ

“Mbebaji hatobeba mzigo wa mwengine.” 35:18

Akasema: “Mimi nakueleza kutoka kwa Abu Muusa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wewe unasema hivi! Je, tunadanganya? Ninaapa kwa Allaah ya kwamba hatukumsemea uogo Abu Muusa wala Abu Muusa hakumsemea uongo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Ameipokea Ahmad.

al-Mughiyrah bin Shu´bah ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Kunisingizia uongo sio kama kumsingizia mtu mwengine. Yule mwenye kunisemea uongo kwa kukusudia basi ajiandalie makazi yake Motoni.” Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Yule ambaye kunafanywa maombolezo kwa ajili yake anaadhibiwa kwa kile anachoombolezewa kwacho.”

Ameipokea al-Bukhaariy, na ni matamshi yake, na Muslim.

an-Nu´maan bin Bashiyr amesema:

“´Abdullaah bin Rawaahah alizimia na dada yake ´Amrah akapiga ukelele kwa kulia na akaanza kusema: “Bwana wangu!” na mambo mengine. Alipopata fahamu akasema: “Hakuna kitu ulichosema isipokuwa niliulizwa: “Ni kweli uko hivo?” Alipokufa akaacha kulia.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

at-Tirmidhiy amepokea katika “al-Jaami´” yake kupitia kwa Abu Muusa ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna maiti anayekufa ambapo walizi wake husema: “Bwana wangu!” na mfano wa hayo isipokuwa Malaika wawili huwakilishwa kumtikisa kifuani na kusema: “Ni kweli uko hivo?”

at-Tirmidhiy amesema:

“Hadiyth ni nzuri na geni.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 51-52
  • Imechapishwa: 14/10/2016