4 – Kubainisha tabia na sifa ambazo walinganizi wanatakiwa kujipamba nazo na kupita juu yake

Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameweka wazi tabia na sifa ambazo walinganizi wanatakiwa kupambika nazo katika Aayah nyingi maeneo mengi katika Kitabu kitukufu. Miongoni mwazo:

1 – Ikhlaasw. Ni lazima kwa mlinganizi awe mwenye kumtakasia nia Allaah (´Azza wa Jall). Si mwenye kutaka kujionyesha, kutaka kusikika wala kusifiwa na watu. Hakika si venginevyo analingania kwa Allaah kwa sababu anataka kuona uso wa Allaah (´Azza wa Jall). Amesema (Subhaanah):

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah.”[1]

وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّهِ

“Na nani mwenye kauli nzuri zaidi kuliko yule anayelingania watu kwa Allaah… ”[2]

Kwa hivyo ni lazima kwako kumtakasia nia Allaah. Hii ni tabia muhimu zaidi. Hii ndio sifa kuu zaidi kwamba iwe katika ulinganizi wako unataka kuona uso wa Allaah na Nyumba ya Aakhirah.

2 – Uwe juu ya ubainifu katika ulinganizi wako. Nikikusudia juu ya elimu. Usiwe mjinga katika kile unacholingania:

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ

“Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah, juu ya ujuzi na umaizi.”

Ni lazima kuwa na elimu. Elimu ni faradhi. Tahadhari kulingania juu ya ujinga na tahadhari kuzungumza kwa usiyoyajua. Mjinga anabomoa na wala hajengi na anaharibu na wala hatengenezi. Kwa hiyo mche Allaah, ee mja wa Allaah! Jihadhari kusema kuhusu Allaah pasi na elimu. Usilinganie katika kitu isipokuwa baada ya kukijua kile alichosema Allaah na Mtume Wake. Ni lazima kuwa na elimu. Ni lazima kwa mwanafunzi na mlinganizi atambue kile anachokilingania na aangalie kile anacholingania kwacho na dalili yake. Haki ikimdhihirikia na akaitambua basi atalingania kwayo. Ni mamoja kitu hicho kiwe cha kufanywa au cha kuachwa. Kwa hivyo alinganie katika kitendo ikiwa ni cha kumtii Allaah na Mtume Wake na alinganie katika kuacha yale aliyokataza Allaah na Mtume Wake kutokana na ubainifu na elimu.

3 – Uwe mpole katika ulinganizi wako, mwenye kufanya urafiki, mvumilivu na mwenye subira. Hivo ndivo walivyofanya Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Jihadhari kufanya haraka. Jihadhari kufanya ukali na ugumu. Lazimiana na subira. Lazimiana na upole na urafiki katika ulinganizi wako. Imeshakutangulia dalili juu ya hayo. Amesema (Jalla wa ´Alaa):

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi.”[3]

فَبِمَا رَحْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ لِنتَ لَهُمْ

”Basi ni kwa rehema kutoka kwa Allaah umekuwa laini kwao… ”[4]

Amesema (Jalla wa ´Alaa) kumwambia Muusa na Haaruun:

فَقُولَا لَهُ قَوْلًا لَّيِّنًا لَّعَلَّهُ يَتَذَكَّرُ أَوْ يَخْشَىٰ

“Mwambieni maneno laini huenda akawaidhika au akaogopa.”[5]

[1] 12:108

[2] 41:33

[3] 16:125

[4] 03:159

[5] 20:44

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 42-45
  • Imechapishwa: 14/06/2023