Wakati alipofariki mtoto mdogo wa Abul-Ahwas, akaja Sufyaan na Zaa-idah kumpa mkono wa pole. Ikawa miongoni mwa mambo ambayo Sufyaan alimwambia:

”Yeye (Subhaanah) amekutunuku na akakupa kile Alichotaka kukupa. Kisha akakutunuku kwa kumchukua Kwake. Amemuweka akiba kwa ajili yako huko Kwake. Kwa hivyo usizingatie neema Yake juu yako kuwa ni msiba. Ni kama kwamba umeungana naye na ukafurahi kwa yeye kukujia.”

al-Haakim Abu ´Abdillâh amesimulia kutoka kwa Abu ´Abdillaah Muhammad bin Ibraahiym al-Mu-adhdhin, ambaye amesema: Nimemsikia Muhammad bin ´Iysaa az-Zaahid akisema:

”Tulipata khabari kuwa mtoto wa kiume wa ´Abdur-Rahmaan bin Mahdiy (Rahimahu Allaah) alifariki, ambapo akafadhaika sana mpaka akaacha kula na kunywa. Khabari hiyo ikamfikia Muhammad bin Idriys ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah), ambapo akamwandikia: ”Jipe pole kama unavowapa pole wengine. Kikemee kitendo chako kama unavyokemea matendo ya wengine. Tambua kuwa masaibu makubwa ni kukosa furaha na kujinyima thawabu. Mtu aseme nini ikiwa ataongezea juu yake kutenda dhambi?”

Kwa wengine tamko limekuja ifuatavyo:

”Kwa hivyo hakikisha, ee ndugu yangu, unachukua fungu lako pindi linapokuwa karibu nawe, kabla ya kuanza kulitafuta wakati lilikuwa mbali nawe. Allaah akupe subira wakati wa masaibu na atulipe thawabu sisi na nyinyi kwa ajili ya subira!”

Imekuja katika upokezi mwingine:

Nafurahi, si kwa sababu sina uaminifu na uhai

lakini ni kwa sababu hivo ndio dini inavyokuwa

Mwenye kufarijiwa habaki baada ya kifo cha maiti wake,

hata yule anayefariji hata kama ataishi mpaka kitambo fulani

Ismaa´iyl bin Haaruun alimpa mkono wa pole bwana mmoja baada ya kufariki mwanawe na akasema:

“Naapa kwa Allaah! Bora ulipwe thawabu juu ya msiba wa wengine kuliko wengine walipwe thawabu juu ya msiba wako.”

Muusa bin al-Mahdiy alimpa rambirambi Abu Ja´far baada ya mtoto wake kuaga dunia na akasema:

“Unafurahishwa na kitendo chake cha kuwa mtihani na inakuhuzunisha yeye kuwa swalah na rehema?”

Akikusudia Aayah:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ مِنْ أَزْوَاجِكُمْ وَأَوْلَادِكُمْ عَدُوًّا لَّكُمْ فَاحْذَرُوهُمْ

”Enyi mlioamini! Hakika kunaweza kuwepo maadui wenu katika wake zenu na watoto wenu; basi tahadharini nao!”[1]

na:

وَلَنَبْلُوَنَّكُم بِشَيْءٍ مِّنَ الْخَوْفِ وَالْجُوعِ وَنَقْصٍ مِّنَ الْأَمْوَالِ وَالْأَنفُسِ وَالثَّمَرَاتِ ۗ وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Bila shaka Tutakujaribuni kwa kitu katika khofu na njaa na upungufu wa mali na nafsi na mazao [katika kazi zenu]. Wabashirie wale wenye kusubiri ambao unapowafika msiba basi husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea – hao zitakuwa juu yao baraka kutoka kwa Mola wao na rehema na hao ndio wenye kuongoka.”[2]

[1] 64:14

[2] 2:155-157

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 107-109
  • Imechapishwa: 22/08/2023