25. Kuhuzunika hakusaidii kitu

´Abdur-Rahmaan bin Ghanm ameeleza kuwa Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Alifariki mwanangu, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaniandikia:

Kutoka kwa Muhammad, Mtume wa Allaah, kwenda kwa Mu´aadh bin Jabal. Amani ya Allaah iwe juu yako. Mimi namshukuru Allaah, ambaye hakuna mungu mwingine wa haki isipokuwa Yeye.

Allaah ayafanye makubwa malipo yako, akutunuku subira na aturuzuku sisi na nyie kushukuru. Hakika nafsi zetu, mali zetu, familia zetu na watoto wetu ni katika zawadi nzuri na mkopo wa Allaah (´Azza wa Jall), ambao Allaah ametufanya kuburudika nao mpaka katika kipindi maalum na baadaye aitwaye katika wakati maalum. Aidha akaamrisha kushukuru wakati anapotoa na kusubiri wakati anapojaribu. Mwanao huyu alikuwa ni miongoni mwa zawadi nzuri na mkopo, ambao Allaah amefanya umestarehe nao kwa furaha. Ukisubiri na ukataraji malipo, basi atakulipa ujira mkubwa. Usiruhusu kukata kwako tamaa kukaporomosha malipo yako, ee Mu´aadh, hivyo ukaja kujutia kile ulichokikosa. Endapo utazingatia malipo ya msiba wako, basi utajua kwamba msiba ni mdogo. Tambua kuwa ni kukata tamaa hakumrudishi yule maiti na wala hakuondoshi huzuni. Kwa hivyo usiwe mwenye masononeko. Kile kilichokupata tayari kilikuwa kimeshakadiriwa. Amani!”[1]

Ameipokea Abu Ahmad al-´Askariy katika “al-Mawaa´id” kupitia kwa Ibn ´Abbaas, kutoka kwa Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anhum). Hata hivyo nimeipokea kupitia kwa ´Aaswim bin Qataadah, kutoka kwa Mahmuud bin Labiyd, kutoka kwa Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh).

Imesemekana kuwa ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) alimpa rambirambi al-Ash´ath bin Qays, juu ya mwanawe aliyekufa, akamwambia:

”Ukikata tamaa juu ya mwanao, una haki ya kufanya hivo upande wa kuunga kizazi. Una kiigizo chema kwa Ya´quub (´alayhis-Salaam) juu ya hilo. Lakini ukisubiri, basi Allaah atalisimamia hilo. Ee al-Ash´ath, ukisubiri, basi utakutana na yale yaliyokadiriwa na pia utalipwa kwa hilo. Na ukikata tamaa, utakutana na yale yaliyokadiriwa na pia utapata dhambi.

Baadhi wameimba mashairi:

Toa rambirambi kwa subira kwa kila mwenye kufa,

kwani subira hufariji masononeko yanayoandama

Usipojiliwaza kwa kusubiri na kutaraji malipo,

utajiliwaza, kama mnyama, muda utavyoenda

Hakuna yeyote awezaye kujilinda kutokana na matamanio

isipokuwa yale ambayo tayari yamekwishapangwa

Imepokelewa kwamba kuna bedui mmoja kutoka katika Banuu Kilaab alimpa mkono wa pole ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz, wakati alipofariki mwanawe ´Abdul-Maalik, akasema:

Mpeni rambirambi kiongozi wa Waumini

kwani, kama mnavoona, anakua mdogo na kuzaliwa

Je, mwanao anatokana na mwingine asiyekuwa Aadam?

Kila mmoja atakunywa kikombe cha mauti

[1] Imezuliwa kwa mujibu wa Ibn-ul-Jawziy katika “al-Mawdhwu´aat” (3/241-242).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 105-107
  • Imechapishwa: 22/08/2023